Rais Samia kushuhudia tamaduni za makabila Ruvuma

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 05:14 PM Sep 19 2024
Rais Samia Suluhu Hassan.
Picha: Ikulu
Rais Samia Suluhu Hassan.

WAKATI Rais Samia akitarajiwa kuwasili mkoani Ruvuma kwa ziara ya kikazi imeelezwa kuwa serikali imewekeza kiasi cha shilingi bilioni 81 kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa bandari ya kisasa ya Mbambabay Wilayani Nyasa Mkoani Ruvuma.

Hayo yalisemwa jana na Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Kanali Ahmed Abbas Ahmed, aliyetemebelea eneo la ujenzi wa bandari hiyo akiambatana na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa kama sehemu ya maandalizi ya mapokezi ya Rais Samia Suluhu Hassan.

Rais Samia anatarajiwa kuwasili mkoani Ruvuma tarehe 23 mwezi huu kwa ziara ya kikazi ambapo pia ataanza kwa kuzindua tamasha la kitaifa la utamaduni litakalofanyika wilayani Songea kuanzia tarehe 20 hadi 23.

Mkuu wa Mkoa alisema ujenzi wa bandari hiyo ukikamilika utasaidia kutoa ajira, kuinua Uchumi, kupeleka na kupokea bidhaa mbalimbali ikiwemo mazao, samaki na bidhaa za viwandani katika Nchi Jirani za Malawi na Msumbiji.

Alisema baada ya kuzindua tamasha la utamaduni Rais Samia  atatembelea wilaya mbalimbali za Mkoa wa Ruvuma kuangalia shughuli mbalimbali za maendeleo ikiwemo miradi ya barabara ambazo zimejengwa kwa viwango vya kimataifa.

Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Kanali Ahmed Abbas Ahmed.
“Barabara zimejengwa kwa viwango  kiasi kwamba ukimleta mtu hawezi kuamini kwamba barabara hizi ziko Ruvuma hasa hii ya kutoka Mbinga  kuja Mbambabay na barabara hii inaenda kufungua uchumi wa mkoa wa Ruvuma kwasababu ni kiunganishi na Malawi na Msumbiji,” alisema

“Tumejiandaa kwa furaha tuliyonayo mkoani kwetu na tunafarijika kuona tumeletewa tamasha kubwa la utamaduni na mkoa wetu umesheheni tamaduni nyingi zikiwemo ngoma na vyakula vya asili kwa hiyo tunaona fahari aje kuona yale mambo mazuri ambayo ameyafanya,” alisema

Tamasha hilo la utamaduni linatarajiwa kuhudhuriwa na watu zaidi ya 5,000 hivyo kuwa fursa kubwa ya kiuchumi kwa wananchi wa mkoa huo kutokana na shughuli za kiuchumi zitakazokuwa zikifanyika kwa siku hizo nne.

Akizungumza na waandishi wa habari Mjini Songea juzi, Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Damas Ndumbaro alisema tamasha hilo litaanza Septemba 20-23, mwaka huu na siku ya kilele kitafanyika uwanja wa majimaji na Rais Samia Suluhu Hassan atakuwa mgeni rasmi.

Alisema tamasha hilo litajumuisha maonesho ya mavazi ya asili ikiwamo kanga, vyakula, ngoma kama vile Mganda na Lizombe. 

Alibainisha kuwa Rais atakutana na wazee wa kimila na kuzungumza nao kwa kuwa mkoa huo unahistoria mbalimbali kama vile vita ya majimaji kwa kutembelea kaburi la halaiki la mashujaa wa majimaji.

“Wanasongea na wanaruvuma tumepewa fursa hii tukifanikisha ndio fursa nyingine tena kwetu, na baada ya hapo Rais ataendelea na ziara mkoa mzima kwenye wilaya zote sita,”alisema.

Alisema Rais Samia atahitimisha ziara yake Septemba 28, mwaka huu kwa kufanya mkutano wa ndani wa Umoja wa Wanawake wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Taifa na mkutano wa hadhara kwa wananchi kwenye uwanja wa majimaji.

Naye, Makamu Mkuu wa Shule ya Sekondari Jenista Mhagama, Meliud Mwampembe, alisema shule hiyo imetoa kipaumbele kwa masuala ya michezo na utamaduni kwa wanafunzi.

“Hili jambo la utamaduni na michezo ni la msingi kwasababu linatunza asili yetu sisi kama watanzania, ninahamasisha sana wananchi kushiriki katika tamasha hili linaloonesha tamaduni zetu lakini na fursa mbalimbali zilizopo Ruvuma,”alisema.