Mchinjita amjibu Rais Samia

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 04:46 PM Sep 19 2024
Makamu Mwenyekiti wa ACT Wazalendo, Isihaka Mchinjita
Picha: Mpigapicha Wetu
Makamu Mwenyekiti wa ACT Wazalendo, Isihaka Mchinjita

Makamu Mwenyekiti wa ACT Wazalendo, Isihaka Mchinjita, akiwa katika Jimbo la Ubungo, jijini Dar es Salaam, kwenye ziara ya chama chake, amemjibu Rais Samia, kufuatia hotuba aliyoitoa wakati wa maadhimisho ya miaka 60 ya Jeshi la Polisi.

Kiongozi huyo wa ACT Wazalendo alieleza kwamba kifo cha aliyekuwa kiongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), marehemu Ali Kibao, ni kifo na tukio la aina yake na lenye sura ya upekee; na hivyo kutokana na mazingira hayo haishangazi kuibua hisia kubwa katika jamii. Hivyo, Mchinjita alisisitiza kwamba Rais Samia anapaswa kuliangalia na kulizingatia jambo hilo kwa aina na namna yake.

"Tukio hili (la Mzee Kibao) ni la aina yake. Watu wengine wote walienda kuchukua na kuteka watu kwa siri. Hawa (waliomteka na kumuua Mzee Kibao) ni wauaji waliopata ujasiri wa kusimamisha basi la abiria. Ndani ya hilo basi kukiwa na askari wa usalama barabarani. (Watu hao) wakamchukua Mtanzania huyu anayejulikana na kesho (Mtanzania huyu) akakutwa ameuwawa. Hii inaonesha kilele cha ujasiri kwa wale wanao ua na kupoteza watu kwenye nchi yetu. (Mauaji haya) hayawezi kuwa sawa sawa na matukio mengine ya kawaida."

Mchinjita aliendelea kusisitiza kwamba kelele zilizopo na zilizoibuka zinatokana na matukio ya utekaji kudumu na kuendelea kwa miaka nane sasa. Kiongozi huyo alieleza kuwa matukio haya yameanza mwaka 2016, huku akikumbushia kwamba kutokana na matukio haya kuwa mengi, Zitto Kabwe, Kiongozi Mstaafu wa ACT Wazalendo aliwasilisha hoja binafsi, katika bunge la awamu ya tano, akiliomba bunge kuunda tume ya uchunguzi, ili kuchunguza hali ya watu kupotea.