Bado siku mbili mbivu, mbichi watakaopata mikopo elimu

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 07:34 AM Sep 19 2024
Mkurugenzi Mtendaji wa bodi hiyo, Dk. Bill Kiwia.
Picha: Mtandao
Mkurugenzi Mtendaji wa bodi hiyo, Dk. Bill Kiwia.

BODI ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imewataka waombaji wa mikopo yake kwa mwaka 2024/25 kufanya masahihisho kwa wale ambao maombi yao yamebainika kuwa na dosari.

HESLB baada ya kufanya uhakiki wa maombi yao, imebaini baadhi ya maombi yanahitaji kufanyiwa masahihisho ili kuruhusu kuendelea kwa hatua inayofuata. 

Taarifa ya HESLB iliyotolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa bodi hiyo, Dk. Bill Kiwia, inasema, "Tunapenda kuwataarifu waombaji wote wa Mikopo ya Elimu ya Juu kuwa tunatarajia kufunga dirisha la masahihisho ya maombi ya mikopo ifikapo tarehe 21 Septemba 2024 (keshokutwa) saa 5:59 usiku.  

"Wote walioomba mikopo wanashauriwa kuingia katika akaunti zao walizotumia kuomba mikopo kuona iwapo wanahitajika kufanya marekebisho.  

"Maombi mapya hayatapokewa kwani dirisha la maombi ya mkopo lilifungwa rasmi Septemba 14, 2024. 

Makundi ya wanafunzi wanaoomba mikopo ni wanafunzi wa shahada za awali (Undergraduate Degrees); wanafunzi wa Stashahada (Diploma); wanafunzi wa Stashahada ya Juu ya Mafunzo ya Uanasheria (Post Graduate Diploma in Legal Practice); na wanafunzi wa shahada za uzamili na uzamivu (Masters and PhD students). 

Bodi hiyo kwa mwaka huu wa masomo imetengewa na serikali Sh. bilioni 787 ambazo zinatarajiwa kuwanufaisha jumla ya wanafunzi 245,000, wakiwamo 80,000 wa mwaka wa kwanza. 

Katika mwaka wa masomo 2023/24, serikali ilitoa mikopo kwa jumla ya wanafunzi 224,056, wakiwamo 78,979 wa mwaka wa kwanza.