'Tabora tunapiga vita mafundi umeme vishoka'

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 04:31 PM Sep 18 2024
Katibu Tawala wa Mkoa wa Tabora, Dk. John Mboya
Picha: Mpigapicha Wetu
Katibu Tawala wa Mkoa wa Tabora, Dk. John Mboya

Katibu Tawala wa Mkoa wa Tabora, Dk. John Mboya, amefungua semina ya siku moja kwa mafundi umeme wa mkoa huo, na kuwasihi kuhakikisha wanakuwa na leseni za ufungaji mifumo ya umeme zinazotolewa na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) kwa mujibu wa Kifungu cha. 8 (h) cha Sheria ya Umeme,Sura Na. 131.

“Kuanzia  leo, mkoa wa Tabora tumepiga vita mafundi vishoka, na ni  imani yangu kwamba baada ya semina hii kila asiye na leseni ataomba leseni ili afanye kazi kwa uhalali, ninawasihi sana tusipoteze fursa hii kwani mkoa wetu una miradi mingi ambayo ni fursa kwa mafundi umeme na kuanzia sasa vishoka wote hawatapewa kazi mpaka pale watakapokuwa na leseni ya EWURA,” alisema. 

Meneja wa EWURA Kanda ya Magharibi, Mhandisi Walter Christopher, amesema semina hiyo iliyowashirikisha mafundi umeme na wadau zaidi ya 150, ililenga kuwajengea uwezo wataalam na wadau hao kuhusu sheria, kanuni, miongozo na utaratibu wa utendaji kwenye shughuli za ufungaji wa mifumo ya umeme. 

Mhandisi Walter Christopher.
Wadau wengine walioshiriki semina hiyo ni Wakala wa Usimamizi wa Ununuzi wa Umma (PPRA), Shirika la Ugavi wa Umeme  nchini (TANESCO), Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Wakala wa Majengo (TBA) na Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA).