Dk.Mwigulu: Soko Kuu la Mwanza kuwa Kariakoo ya Kanda ya Ziwa

By Vitus Audax , Nipashe
Published at 07:57 PM Sep 17 2024
Soko Kuu la Mwanza.
Picha: Vitus Audax
Soko Kuu la Mwanza.

WAZIRI wa Fedha Dk.Mwigulu Nchemba ameeleza kuridhishwa na utekelezaji wa Mradi wa Soko la Kuu la kisasa la Mwanza na kuwa limekidhi vigezo vya Kimataifa hivyo linatarajiwa kuwa kama Soko Kuu la Kimataifa la Kariakoo lililopo jijini Dar es Salaam.

Dk.Nchemba ametoa kauli hiyo mapema leo wakati akikagua ujenzi wa soko hilo ambalo limefikia asilimia 96 likitarajiwa kutumia zaidi ya Sh.bilioni 23 hadi kukamilika kwake.

“Mikataba uliopo baina ya wananchi na Serikali yao ni kuhakikisha tunawaletea maendeleo kwa kutekeleza shughuli na miradi mbalimbali ya kimaendeleo ambavyo ndicho kitu tunachokifanya kwa sasa hivyo wajiandae tu kuanza kupata matunda ya mradi huu muhimu katika uchumi wa kanda ya Ziwa,”amesema Dk.Nchemba.

Aidha amesema serikali inaendelea na utekelezaji wa miradi yote pamoja na kuanzisha mingine lengo ni kuhakikisha wananchi wanapata maendeleo yanayotakiwa.

1

Mbunge wa Jimbo la Nyamagana Stanislaus Mabula amesema utekelezaji wa Mradi huo itasaidia kuongeza mzunguko wa kibiashara na kuwa ni sahihi mzunguko huo utalifanya soko hilo kuwa sawa na Soko Kuu la Kariakoo Dar es salaam kwa mzunguko wa kibiashara pamoja na mapato.

Amesema wakati Mradi huo unapokelewa na Rais Samia Suluhu Hassan zilikuwa zimetolewa zaidi ya Sh.bilioni 1.7 pekee lakini kwa kipindi cha miaka mitatu imepokelewa zaidi ya Sh.bilioni.20.

Alisema awali wafanyabiashara waliokuwepo hawakufika hata 300 lakini kwa sasa watakuwepo wafanyabishara 1400 zaidi ya mara tatu ya wale wa awali na wote waliokuwepo awali wataendelea kunyabiashara zao pamoja na wengine wapya.

Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana Amina Makilagi alisema Wilaya hiyo imepokea zaidi ya Sh.bilioni 350 ambako Sh.bilioni 111 kwaajili ya utekelezaji wa Mradi wa Meli ya MV.Mwanza hapa kazi Tu, Sh.bilioni 23 kwaajili ya soko kuu, Stendi Kuu ambayo imegharimu Sh.bilioni 17 pamoja na utekelezaji wa miradi ya barabara Sh.bilioni 11.
2