Gofu Wanawake yahitimishwa Arusha NBC ikiahidi mazuri zaidi

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 08:22 PM Sep 17 2024
Wadau mbalimbali wa mchezo wa gofu wakiwemo washindi wa mashindano ya gofu ya Tanzania Ladies Open Golf Tournament wakijipongeza na zawadi zao wakati wa hafla fupi ya kuhitimishwa kwa mashindano hayo ya siku tatu yaliyohitimiswa mwishoni mwa wiki.
Picha:Mpigapicha Wetu
Wadau mbalimbali wa mchezo wa gofu wakiwemo washindi wa mashindano ya gofu ya Tanzania Ladies Open Golf Tournament wakijipongeza na zawadi zao wakati wa hafla fupi ya kuhitimishwa kwa mashindano hayo ya siku tatu yaliyohitimiswa mwishoni mwa wiki.

MASHINDANO ya siku tatu ya Gofu yajulikanayo kama Tanzania Ladies Open Golf Tournament, yamehitimishwa mwishoni mwa wiki jijini Arusha huku wadhamini wakuu wa mashindano hayo, Benki ya Taifa ya Biashara (NBC), wakiahidi kuendelea kuyaboresha zaidi ili kuyaongozea ubora na ushindani utakaowavutia washiriki wengi kutoka ndani na nje ya nchi.

Mashindano hayo ya siku tatu yaliyofanyika kwenye viwanja vya Klabu ya Gofu ya Gymkhana jijini Arusha, yalifanikiwa kuvutia washiriki kutoka klabu zote za mchezo huo hapa nchini sambamba na washiriki wengine kutoka katika mataifa ya Kenya na Uganda huku  mchezaji Mkenya Mercy Nyanchama akiibuka mshindi wa jumla.

Akizungumza kwenye hafla fupi ya kukabidhi zawadi kwa washindi mbalimbali wa mashindano hayo, Meneja Mahusiano wa Benki ya NBC,  Gerald Tarimo, pamoja na kuwapongeza washiriki na washindi mbalimbali wa mashindano hayo, alisema benki hiyo itaendelea kuyaunga mkono ikiwamo kuyaboresha zaidi ikiwa ni sehemu ya jitihada zake katika kuchochea ushiriki wa wanawake katika michezo.

“Pamoja na kuvutiwa na idadi kubwa ya washiriki kwenye mashindano haya, zaidi tumevutiwa na maandalizi mazuri yaliyochochea ushindani uliokusudiwa kwa kuwa washiriki hawakuwa na changamoto ambazo zingeweza kuathiri uwezo wao kimchezo.

‘’Mara nyingi NBC tumekuwa tukikabidhi zawadi mbalimbali kwa washindi wa kiume zikiwamo klabu za mpira wa miguu kwenye ligi tatu tunazozidhamini nchini ikiwamo Ligi Kuu ya NBC, hivyo tunapopata nafasi ya kufurahia na kukabidhi zawadi kwa washindi wanawake kama leo hivi kwetu ni furaha pia,’’ alisema.

Kwa mujibu wa Tarimo, kutokana na mafanikio yanayoendelea kuonekana kupitia udhamini wa benki hiyo kwenye mchezo wa gofu nchini, NBC inadhamiria kuendelea kushirikiana na wadau mbalimbali wa mchezo huo kufanikisha mashindano mbalimbali kwa viwango vyenye ubora zaidi ili kuchochea ukuaji na kuibua vipaji vipya hususan kwa watoto.

Kwa upande wa rais wa Chama cha Gofu cha Wanawake Tanzania (TLGU), Queen Siraki, pamoja na kuwapongeza washiriki na washindi mbalimbali wa mashindano hayo wakiwamo wale waliotoka nje ya nchi, pia aliwashukuru wadau mbalimbali waliofanikisha mashindano ikiwa ni pamoja na mdhamini mkuu wa mashindano hayo Benki ya NBC.

Aidha, Siraki alitoa wito kwa jamii hususan wanawake kushiriki kwa wingi kwenye mchezo huo unaojiongezea umaarufu hapa nchini huku akiwasihi wapuuzie dhana iliyojengeka kwa muda mrefu kuwa mchezo wa gofu ni mahususi tu kwa watu wenye kipato kikubwa kwenye jamii au wanaume tu.

“Maandalizi mazuri yaliyohusisha pia zawadi nzuri na zenye viwango kama ilivyokuwa kwenye mashindano haya ndio chachu ya kuendelea kuvutia zaidi washiriki kutoka ndani na nje ya nchi na kwenye hilo tunawashukuru sana wadhamini wetu hususan Benki ya NBC. Ni matumaini yetu wataendelea kutuunga mkono zaidi mashindano yajayo kwa kuwa tunatazamia kuwa na mambo mazuri zaidi kutokana na mwamko mkubwa unaoendelea kushuhudiwa ukihusisha ongezeko kubwa la wachezaji na vipaji vipya vya mchezo huu,’’ alisema.

Wadau mbalimbali wa mchezo wa gofu wakiwemo washindi wa mashindano ya gofu ya Tanzania Ladies Open Golf Tournament wakijipongeza na zawadi zao wakati wa hafla fupi ya kuhitimishwa kwa mashindano hayo ya siku tatu yaliyohitimiswa mwishoni mwa wiki jijini Arusha. Benki ya NBC ilikuwa mdhamini Mkuu wa mashindano hayo yaliyofanyika kwenye viwanja vya klabu ya gofu ya Gymkhana jijini Arusha.