Bodi mpya Hospitali ya Rufani Shinyanga yazinduliwa

By Marco Maduhu , Nipashe
Published at 01:01 PM Feb 12 2025
Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga, CP Salum Hamduni, akizundua Bodi Mpya ya Hospitali ya Rufaani ya Mkoa wa Shinyanga
Picha: Marco Maduhu
Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga, CP Salum Hamduni, akizundua Bodi Mpya ya Hospitali ya Rufaani ya Mkoa wa Shinyanga

KATIBU Tawala wa Mkoa wa Shinyanga, CP Salum Hamduni, amezindua bodi mpya ya ushauri ya Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Shinyanga.

Ameeleza kwamba bodi hiyo ni ya muhimu katika uendeshaji wa huduma za afya na kutoa huduma bora ya matibabu kwa wananchi. Bodi hiyo imezinduliwa jana, Februari 11, 2025.

Hamduni amewapongeza wajumbe kwa kuteuliwa na Waziri wa Afya, kuisimamia hospitali hiyo, na kwamba kazi ya bodi ni kuishauri menejimenti katika utendaji kazi, ili kuboresha huduma za afya.

“Bodi ya ushauri ya Hospitali ya Rufani ya Mkoa, ni chombo muhimu sana katika uendeshaji wa huduma za afya za Hospitali. Ni kiungo kinachowaunganisha wananchi na serikali yao na kuboresha utoaji wa huduma,” amesema Hamduni.

“Kazi kubwa ya bodi ni kuisimamia karibu sana menejimenti ya hospitali katika utekelezaji wa majukumu yake, kimsingi menejmenti ya hospitali inawajibika moja kwa moja kwa bodi, hivyo wajumbe tumieni taaluma zenu kuisaidia hospitali katika uendeshaji wa huduma za afya,” ameongeza.

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Dk. Yudas Ndungile, amesema bodi hiyo ni wawakilishi wa watumiaji wa huduma ambayo inatolewa hospitali na wakisikia kuna malalamiko na manun’guniko juu ya utoaji wa huduma, wawasiliane na menejimenti ili kutatuliwa.

Mwakilishi kutoka Wizara ya Afya, Dk. Fadhili Kibaya, amesema bodi hiyo itadumu kwa muda wa miaka mitatu na kazi yake ni kuhakikisha hospitali inatoa huduma bora za matibabu kwa wananchi.

Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Shinyanga, Dk. Luzila John, amesema hospitali hiyo ilianzishwa rasmi mwaka 1947, ikiwa kama kituo cha kutolea huduma, baada ya Vita ya Kuu ya Pili ya Dunia, ilijengwa kwa nguvu za wananchi.

Bodi mpya Hospitali ya Rufani Shinyanga yazinduliwa
Amesema mwaka 1974 ilipanda daraja kuwa Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Shinyanga na mwaka 2010 ikatangazwa rasmi na kwamba mwaka 2014 ilianza kujengwa hospitali mpya Kata ya Mwawaza na huduma za matibabu zilianza kutolewa mwaka 2022.

“Hospitali yetu inaweza kutoa huduma kwa wagonjwa wa nje 58,319 na mwaka jana; wagonjwa waliolazwa ni 6,787; akinamama waliojifungua 1,421. Tunampongeza Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kuboresha huduma za afya hospitali hapa,” amesema Dk. Luzila.

Pia, amepongeza Rais Samia kwa kuamua kutengeneza miundombinu ya barabara ya kufika katika hospitali hiyo kwa kiwango cha lami, na zabuni yake imetengazwa juzi.

Ameomba mchakato wa ujenzi wa barabara hiyo uharakishwe na ujenzi uanze mara moja na kuondoa usumbufu kwa wagonjwa.

Aidha, ameipongeza bodi hiyo na kuahidi kwamba watafanya kazi kwa kushirikiana kwa ukaribu, ili kuboresha huduma za afya katika hospitali hiyo.

Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya hospitali hiyo, Dk. John Majigwa, amesema watafanya kazi kwa nguvu zote, ili kuinua huduma za afya hospitalini hapo.