Chanika tishio kwa ukatili dhidi ya watoto

By Christina Mwakangale , Nipashe
Published at 06:21 PM Jul 02 2024
Kaimu Inspekta Majaliwa Kilowa kutoka kituo cha Polisi Kata ya Chanika,akizungumza.
Picha: Mpigapicha Wetu
Kaimu Inspekta Majaliwa Kilowa kutoka kituo cha Polisi Kata ya Chanika,akizungumza.

WAZAZI na walezi wameaswa, kutelekeza malezi kwa jamii, jambo linalosababisha watoto kufanyiwa vitendo vya ukatili kama vile ulawiti.

Kaimu Inspekta Majaliwa Kilowa kutoka kituo cha Polisi Kata ya Chanika, jijini Dar es Salaam, aliyasema hayo mwishoni mwa wiki, kwa niaba ya OCD Awadhi Chicco.

Akizungumza kwenye maadhimisho ya Siku ya mtoto wa Afrika, sambamba na uzinduzi wa shirika la Tumanyile Relief Foundation (TUREFO), alisema taarifa za ukatili dhidi ya watoto hufikishwa kituoni hapo.

“Wazazi waangalie watoto wenu. Pia angalieni namna migogoro ndani ya familia, ili isiwaathiri watoto. Wazazi na walezi walindeni watoto wenu na kukaa karibu na mtoto.

“Tuache mila potofu ni mbaya, watoto wapelekwe shule, vilevile ajira hazitakiwi kwa watoto. Kuna ripoti nyingi, zikiongezeka kuhusu ukatili wa watoto Chanika,” alifafanua Inspekta Majaliwa.

Ofisa Maendeleo ya Jamii, Robert Zabron, akizungumza kwa niaba ya Mtendaji wa Kata hiyo, alisema kuanzishwa kwa shirika hilo ambalo limejikita kutoa ushauri na utetezi, itasaidia kupunguza ukatili kwa watoto.

“Mtoto ana haki ya kuwa usalama, ulinzi. Watoto wanapata shida, Chanika tunaongoza kwa matukio ya ulawiti unatisha hapa Chanika,” alisema Zabron.

Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa TUREFO, Rachel Malimbwi, alisema lengo la kuanzishwa shirika hilo lenye maono ya waanzilishi 10 ni kuinua kiwango cha kiuchumi katika jamii, hasa kwa wenye mahitaji zaidi.

Alisema pia limejikita kutoa msaada wa dharura, ushauri na elimu kwa wototo na vijana kuhusu namna bora ya kuenenda kijamii na kuwa wazalendo.