Dk.Mpango aielekeza Wizara ya Madini kusimamia madini mkakati

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 06:14 PM Aug 22 2024
 Dk.Mpango aielekeza Wizara ya Madini kusimamia madini mkakati.
Picha:Mpigapicha Wetu
Dk.Mpango aielekeza Wizara ya Madini kusimamia madini mkakati.

Makamu wa Rais Dk. Philip Mpango ameitaka Wizara ya Madini kuhakisha inasimamia vyema uvunaji wa madini ya kimkakati ili nchi iweze kunufaika nayo.

Dk. Mpango ameyasema hayo leo Katika eneo la Mpwayungu, Wilaya ya Chamwino-Dodoma wakati akihitimisha ziara ya siku 4 ya Mkoa wa Dodoma.

“Mwenyezi Mungu ametujaalia rasilimali hii ya madini mkakati yenye mahitaji makubwa sana Duniani," amesema Dk. Mpango.

Amesema Mkoa wa Dodoma umebarikiwa kuwa na madini  mkakati kwa wingi na aina tofauti tofauti, na kueleza kuwa ni  lazima rasilimali  hiyo ikatafsirike katika maendeleo ya wananchi wa Dodoma na Tanzania kwa ujumla.

"Wizara ya Madini hakikisheni mnaweka mpango mzuri wa usimamizi wa rasilimali hii kwa manufaa ya Taifa na kwa manufaa ya vizazi vijavyo” amesema Dk. Mpango.

Akiwasilisha salamu za Wizara Waziri wa Madini Anthony Mavunde amemwahidi Dk.Mpango kuyafanyia kazi maelekezo yote na kwasasa Wizara inakamilisha andiko la mkakati wa usimamizi na uvunaji wa madini hayo ili yalete faida kwa nchi kwa  kuchochea uchumi na kuendeleza sekta ya madini.

Mavunde ametumia fursa hiyo kutoa maelekezo kwa Maafisa Madini Wakazi kuhakikisha wanasimamia ipasavyo maeneo yenye uchimbaji wa madini mkakati ili manufaa yake yaonekane kwa Taifa.