JK aihakikishia Nigeria uhusiano kibiashara, diplomasia

By Joyce Lameck , Nipashe
Published at 09:07 AM Aug 22 2024
Rais mstaafu, Dk. Jakaya Kikwete, akifurahia jambo na mwenyeji wake, Makamu wa Rais wa Nigeria, Kashim Shettima, walipokutana na kufanya mazungumzo katika Ikulu ya Rais, Abuja, jana.
PICHA: OFISI YA RAIS MSTAAFU
Rais mstaafu, Dk. Jakaya Kikwete, akifurahia jambo na mwenyeji wake, Makamu wa Rais wa Nigeria, Kashim Shettima, walipokutana na kufanya mazungumzo katika Ikulu ya Rais, Abuja, jana.

RAIS mstaafu wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete ameeleza utayari wa Tanzania kuimarisha uhusiano wake wa kibiashara, kidiplomasia na Nigeria.

Aidha, amesema anatambua umuhimu wa urafiki kati ya mataifa hayo mawili na kusisitiza dhamira ya Tanzania kuzidisha uhusiano huo.

Kwa mujibu wa taarifa kwa umma iliyotolewa jana, Kikwete aliyasema hayo juzi wakati wa mkutano kati yake na Makamu wa Rais wa Nigeria, Kashim Shettima, Ikulu ya Rais, Abuja.

Aidha, alisema anatambua jukumu la Chuo cha Ulinzi cha Taifa cha Nigeria katika kutoa mafunzo kwa wanajeshi wa Tanzania. 

Alisema ushirikiano huo ni sehemu muhimu ya uhusiano wa ulinzi na kidiplomasia kati ya nchi hizo mbili, akieleza kuridhishwa kwa ushirikiano wa kina na mpana katika maeneo haya.

Makamu wa Rais wa Nigeria, Shettima, alitoa wito wa kuimarisha ushirikiano kati ya Nigeria na Tanzania, akisisitiza umuhimu wa ujumuishaji wa kikanda na juhudi za pamoja ili kufanikisha ukuaji na umoja wa bara.

Alisema nchi zote mbili zina uhusiano wa muda mrefu, hasa kama nchi za mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya ubaguzi wa rangi na ukoloni.

Hata hivyo, alisisitiza haja ya kujenga historia hiyo ya pamoja ili kukuza uhusiano imara wa kiuchumi na kijamii, hasa ndani ya mfumo wa Eneo Huru la Biashara la Afrika (AfCFTA), “Tanzania ni moja ya hadithi za mafanikio za Afrika,” alisema Shettima.

“Kuanzia Julius Nyerere hadi Samia Suluhu Hassan, Tanzania imebarikiwa kuwa na viongozi bora na kuwa taifa hilo ni mfano wa matumaini na utulivu katika Afrika Mashariki.”

Makamu wa Rais wa Nigeria, alionesha furaha kwa kugundulika kwa akiba kubwa ya gesi, alisema Tanzania iko kwenye njia ya maendeleo ya haraka, jambo ambalo linafungua fursa za ushirikiano wa kina kati ya mataifa hayo mawili.

“Iwapo mataifa muhimu ya Afrika kama Nigeria na Tanzania yatapata mafanikio, bara zima litanufaika,” alisisitiza.

Pia, aliipongeza Serikali ya Tanzania kwa kuunga mkono biashara za Nigeria zinazofanya kazi ndani ya mipaka yake, akitaja mafanikio ya kampuni kama United Bank for Africa, Guarantee Trust Bank na Dangote Group.

Alisema kuna uwezekano wa kuongezeka kwa biashara na uwekezaji kati ya nchi hizo mbili, jambo ambalo litazidi kuimarisha uhusiano wao wa kiuchumi.