JKCI mbioni kufungua kitengo cha moyo Arusha

By Beatrice Shayo , Nipashe
Published at 09:49 AM Jul 01 2024
MKURUGENZI Mtendaji wa Taasisi ya Jakaya Kikwete (JKCI), Dk. Peter Kisenge.
Picha: Mtandao
MKURUGENZI Mtendaji wa Taasisi ya Jakaya Kikwete (JKCI), Dk. Peter Kisenge.

MKURUGENZI Mtendaji wa Taasisi ya Jakaya Kikwete (JKCI), Dk. Peter Kisenge, amesema wapo katika mchakato wa kuanzisha kitengo cha moyo Mkoa wa Arusha ili kutoa matibabu kwa ukaribu zaidi.

Kisenge aliyasema hayo jana mkoani hapa wakati akizungumza na wananchi waliojitokeza kwenye kambi ya matibabu bure inayotarajia kumalizika leo, huku akieleza kuwa kituo hicho kitakuwa na mitambo mikubwa ya upasuaji.

“Tutakuwa na mitambo mikubwa ya upasuaji wa moyo na kuweka klabu, tayari fedha tumeanza kuzitafuta tutakuwa na kitengo cha moyo na kuwatibia mikoa yote ya pembeni,” alisema Dk. Kisenge.

Alisema kwa matukio aliyoyaona katika kambi hiyo, magonjwa ya moyo kwa Mkoa wa Arusha yana takwimu kubwa na kuanzia Septemba watakuwa na kliniki itakayoshirikiana na wataalamu wa Jiji la Arusha kutoa huduma.

Aidha, aliwaomba wananchi kufanya mazoezi mara tatu kwa wiki kwa kuwa yatasaidia kuwalinda wasipate maradhi ya ugonjwa wa moyo.

Alisema kwa upande wa moyo wamewaona zaidi ya watu 1,500 kati ya hao asilimia 40 wamekutwa na matatizo mbalimbali na wengine wana shida ya umeme wa moyo.

“Kuna mgonjwa ambaye nilimkuta ana mapigo ya moyo chini ya 39 alikuwa hajijui. Mwanadamu ili aweze kuishi anatakiwa mapigo yake yaanzie 60 na kuendelea yeye alikuwa na 39 tumemkimbiza Dar es Salaam kwa matibabu zaidi,” alisema.

Kwa mujibu wa Dk. Kisenge, kama asingefika katika kambi hiyo huenda angepoteza maisha ghafla na watu wa aina hiyo wengi hupoteza maisha wakiwa wamelala.

Aidha, alisema wagonjwa 183 waliokuwa na matatizo ya moyo wamepelekwa JKCI na wote wanalipiwa na Rais Samia Suluhu Hassan na hakuna atakayekosa huduma.

Aidha, wamewaona watoto 150 waliokuwa na matatizo mbalimbali kati yao 53 wanatakiwa kufanyiwa upasuaji mkubwa wa moyo.

Alisema watoto hao watapelekwa Mkoa wa Dar es Salaam kwa ajili ya upasuaji na kila mtoto mmoja kufanyiwa upasuaji ni Sh. milioni 12, matibabu hayo yatagharamiwa na Rais Samia.

Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda, alisema amepata faraja kubwa kutokana na siku saba za kutoa matibabu na kuwafikia zaidi ya watu 30,000.

Makonda alisema wamekubaliana na madaktari wa mkoa na timu inayotoa huduma kuongeza siku moja kwa ajili ya wale ambao wana namba wapatiwe huduma.

“Itakuwa haina maana mwananchi amekuja tangu Alhamisi na wengine wamelala kwenye huu uwanja warudishwe nyumbani bila kutibiwa hili sio jambo la haraka yaani unaingia na kutibiwa kuna baadhi ya sampuli zimepelekwa mkoani wa Dar es Salaam ili wapatiwe majibu,” alisema.

Aidha, Makonda aliahidi kutafuta wadau wamsaidie viti mwendo kwa ajili ya watu 1,000 na watafikiwa kwenye kila wilaya.