KITABU: Profesa Janabi: Huu ndio uhusiano wa sukari na kifo

By Christina Mwakangale , Nipashe
Published at 09:39 AM Aug 22 2024
Prof. Mohamed Janabi.
Picha: Mtandao
Prof. Mohamed Janabi.

MKURUGENZI Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Prof. Mohamed Janabi, amesema jamii inapaswa kuondokana na dhana kwamba mtu mnene na mwenye kitambi ndiye mwenye uchumi mzuri.

Anasema ni dhahiri kwamba unene uliopitiliza si kielelezo cha mafanikio, bali hatari ya kiafya na dalili ya magonjwa yasiyoambukiza (NCD). 

Bingwa huyo bobezi katika magonjwa ya moyo na Daktari Mkurugenzi katika Shirika lililo la kiserikali la Madaktari wa Afrika lenye asili yake Marekani, anabainisha hayo katika kitabu chake cha 'Mtindo wa Maisha na Afya Yako'. 

"Dhana kuwa unene ndio dalili ya uchumi binafsi na afya njema, ni potofu, Itachukua muda mrefu sana kwa watu kuja kuelewa. Kama ilivyoelezwa kwa mifano, kitambi kinahusishwa na magonjwa mengi yasiyoambukiza. 

"Utafiti mbalimbali wa wataalamu wa sayansi na hasa wa tiba, umethibitisha kuwapo uhusiano wa moja kwa moja kati ya ulaji wa sukari, wanga kwa wingi na vifo (positive correlation)," anasema. 

Prof. Janabi anafafanua kwamba, viwango vya vifo kati ya mwaka 1905 hadi mwaka 1950, vilipanda na kushuka, kwa idadi ya watu wanaoathirika katika kipindi husika. 

"Wakati wa ulaji mkubwa wa sukari na wanga, pia kulikuwa na vifo vingi, Hali kadhalika, wakati wa uhaba ambao ulisababisha ulaji sukari na wanga kupungua, vifo navyo vilipungua. 

"Kwa mfano, wakati wa Vita Kuu ya Dunia kati ya mwaka 1914 hadi 1918 (WWI), uhaba wa sukari na wanga kutokana na sababu kama vile uzalishaji kuwa chini, ulipunguza ulaji wake. 

"Hali Kadhalika wakati wa Vita Kuu ya Pili ya Dunia (WWII), kati ya mwaka 1938 hadi 1945, uhaba ulisababisha ulaji wa chini wa sukari na wanga," anasema. 

Prof. Janabi anasema kuwa katika utafiti wao, wataalamu waliona kuwako kwa mfanano wakati wa vita hivyo yaani WWl na WWIl, kwa kuangalia idadi ya vifo na ulaji wa sukari. 

"Kukiwa na ulaji mdogo wa sukari na wanga, idadi ya vifo vinapungua, lakini ulaji sukari na wanga ukiongezeka kunakuwa na vifo vingi," anaonya bingwa huyo. 

Prof. Janabi anashauri jamii ijikite katika mlo wa vyakula vya protini na mboga za majani zaidi, kutumia mafuta ya mizeituni, kula matunda kwa wingi kama vile maparachichi. 

"Fanya mazoezi mara kwa mara, walau kwa siku tembea hatua 10,000. Dhibiti uzito wa mwili wako, kwa kuwa na uzito unaokubalika kulingana na BMI. 

"Acha kula vitafunwa mara nyingi kwa siku, kwa sababu ulaji wa vitu vidogo (snacks) kati ya milo, ndiyo chanzo cha kuongezeka kwa insulini mwilini," anaonya. 

Prof. Janabi anasema kuwa kwa kuzingatia ulaji huo, mwili utahisi njaa kidogo kwa siku na matokeo yake, hautazalisha insulini nyingi ambayo ndiyo chanzo cha matatizo ya magonjwa mengine mengi.