Makalla: Makundi yanaigharimu CCM lazima yavunjwe

By Romana Mallya , Nipashe
Published at 02:47 PM Jul 06 2024
KATIBU wa NEC Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM Taifa CPA Amos Makalla
PICHA: Romana Mallya
KATIBU wa NEC Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM Taifa CPA Amos Makalla

KATIBU wa NEC Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM Taifa CPA Amos Makalla, amewataka wanachama wa chama hicho kujiweka sawa kuelekea uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024 na Uchaguzi Mkuu mwakani kwa kuanza kuvunja makundi ambayo yamekuwa yakikigharimu chama hicho.

Kadhalika amekemea baadhi ya wana CCM kujiweka mbali na upangaji wa safu za viongozi kwa sababu ni kinyume na taratibu za chama hicho.

Makalla ambaye pia ni mlezi wa Chama Cha Mapindizi Mkoa wa Dar es Salaam, ametoa kauli hiyo leo baada ya kupokewa katika ukumbi wa Diamond Jubilee tayari kwa kuanza ziara yake ya siku saba mkoani humo.

"Chakula cha wanasiasa ni watu kwenye hili mmenitia nguvu na tumeanza vizuri, tuendelee hivi hivi kwani ndio kwanza tumeanza, lakini wakati nimeteuliwa kwenye Uenezi nilisema nimerudi nyumbani na leo nimepewa nafasi ya ulezi wa Mkoa wa Dar es Salaam sehemu ambayo nimeanzia siasa mpaka sasa narudia kusema nimerudi nyumbani.

"Nimekuja kwanza mpokee salamu za Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Taifa anawasalimia sana," amesema.

Makalla amesema amekuja Dar es Salaam kama Katibu wa NEC Itikadi na Uenezi na Mlezi kukagua uhai wa CCM kwa maana walivyozunguka mikoa 11 wameona wanaCCM wapo tayari.

Katika hatua nyingine, Makalla amesema kuwa CCM haiwezi kujitenga na matatizo ya wananchi na hivyo ametumia mkutano huo kuwambusha watendaji wajibu wao.

Amewataka watendaji wa serikali wakiwamo wakuu wa mikoa, wilaya na wakurugenzi kuendelea na utaratibu wa kutenga muda ili kusikiliza na kutatua kero mbalimbali za wananchi

Aidha, Makalla amesema CCM kushinda uchaguzi ni namba kubwa na wao kushinda ni lazima.

"Niseme niseme leo  nawajuza kuwa Chama Cha Mapinduzi ndio chama namba tisa chenye wanachama wengi duniani na namba moja Afrika na bado hatufungi milango kwa wanachama wapya, kwani uchaguzi ni namba tunavyokuwa na namba kubwa ndio ushindi wetu," amesema.

Amesema mpaka sasa CCM kuna wanachama zaidi ya milioni 10, hivyo hapo tu hakuna wakuwashinda na wajue mabalozi ndio wana watu wengi hivyi waendelee kujiandikisha ili kupata wanachama wengi na kushinda kwa urahisi zaidi.

Chama cha Mapinduzi ni chama cha umoja na mshikamano, bado ninasisitiza uchaguzi unapoisha basi umeisha, masuala ya makundi lazima tuyavunje," anasema.