Manji azikwa Marekani, Yanga wamlilia

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 12:48 PM Jul 02 2024
Hapa ndipo mwili wa aliyekuwa Mwenyekiti na Mfadhili wa klabu ya Yanga SC, Yusuph Manji ulipozikwa. Mazishi ya Manji yalifanyika Jana Julai 1, 2024 huko Orlando, Florida Nchini Marekani.
Picha Digital
Hapa ndipo mwili wa aliyekuwa Mwenyekiti na Mfadhili wa klabu ya Yanga SC, Yusuph Manji ulipozikwa. Mazishi ya Manji yalifanyika Jana Julai 1, 2024 huko Orlando, Florida Nchini Marekani.

ALIYEKUWA mdhamini, mfadhili na Mwenyekiti wa Klabu ya Yanga, Yusuph Manji, aliyefariki Juni 29, mwaka huu jijini Florida, Marekani, amezikwa jana nchini humo.

Aidha, Klabu ya Yanga imesikitishwa na kifo hicho, ikisema alikuwa ni mwanamapinduzi wa soka nchini na shujaa aliyependa maendeleo ya sekta hiyo.

Taarifa iliyotolewa jana na mtoto wa marehemu, Mehbub Manji, ilieleza kuwa angezikwa jana saa tisa alasiri Orlando Florida karibu na sehemu aliyozikwa baba yake. 

Wakati huo huo, Klabu ya Yanga imesema Manji alikuwa  mmoja wa watu waliobadilisha Soka la Tanzania kutoka kuonekana kama la ridhaa zaidi na kuwa la kulipwa. 

Ofisa Habari wa Klabu hiyo, Ali Kamwe alisema klabu ya Yanga imesikitishwa na kifo cha mfanyabiashara huyo maarufu ambaye alitumia nguvu, pesa na ushawishi wake kuboresha timu hiyo na kubadilisha mfumo wa uendeshwaji wa kuwa wa kisasa. 

Alisema kwa wanachama wa klabu hiyo, Manji alikuwa ni  mwanamapinduzi mkubwa katika mpira wa miguu ambaye alishiriki kwa hali ya mali kuhakikisha klabu  inakuwa bora ndani na nje ya uwanja.

 “Kwa niaba ya uongozi wa Yanga, Kamati ya Utendaji, tumepokea kwa masikitiko taarifa hii ya kifo cha Yusuph Manji ambaye alikuwa mdhamini, mfadhili na mwenyekiti wa klabu yetu.

 “Hadi umauti unamkuta alikuwa mwanachama wa klabu yetu, hivyo tunatoa pole kwa ndugu, jamaa marafiki na wanamichezo wote kwa ujumla kwa sababu huu siyo msiba wetu tu, unaigusa sekta ya michezo,” alisema Kamwe. 

Akizungumza kutoka nchini Uholanzi, mmiliki wa klabu ya African Lyon, Rahim Zamunda, alisema Manji pamoja na kutoka Yanga, bado aliendelea kuwa na mapenzi na klabu hiyo na alisafiri kutoka nchini Marekani kwenda Afrika Kusini kuangalia mechi ya marudiano ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika katika ya timu yake dhidi ya Mamelodi Sundowns. 

Taarifa za kifo hicho cha Mkurugenzi huyo wa Kampuni ya  Quality Group Limited, na  Diwani wa zamani wa Kata ya Mbagala Kuu kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), zilitolewa juzi usiku na mtoto wake. 

Mfanyabiashara huyo atakumbukwa zaidi na wanachama na mashabiki wa timu hiyo kwa kumaliza mgogoro wa muda mrefu kati ya makundi mawili hasimu, Yanga Asili na Yanga Kampuni na kuirudisha kwenye hadhi yake. 

Aliingia Yanga mwaka 2006 kama mdhamini kupitia kampuni yake moja ya bahati nasibu, baadaye mfadhili Mkuu wa klabu, kabla ya kuwa Mwenyekiti. Moja ya wachezaji ambao timu hiyo iliwasajili kwa kishindo ni kutoka kwa mahasimu wao wa jadi Simba, Emmanuel Okwi, Kelvin Yondani, Juma Kaseja. 

Kisha ikawapora mchezaji, Mbuyu Twite ambaye alikuwa ameshatangazwa kuwachezea  Wekundu wa Msimbazi hao kutokea, APR ya Rwanda.