Ni Taharuki: Utekaji washika kasi Kigoma

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 10:12 AM Jul 02 2024
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma, Philemon Makungu.
Picha: Maktaba
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma, Philemon Makungu.

MATUKIO ya watu kutekwa kwa kutumia magari na watu wenye silaha za moto (bastola) katika Kata ya Kibirizi na maeneo mengine mkoani Kigoma, yamesababisha taharuki.

Matukio hayo yanadaiwa kushika kasi kuanzia mwezi Mei mwaka huu, huku watekaji wakidaiwa pia kutumia sindano za dawa ya usingizi.

Imedaiwa kuwa watekaji hao wanapofanikiwa kuteka hudai fedha kwa ndugu wa watu hao, huku waathirika wakishindwa kutoa ripoti na kuzua maswali.

Ramadhan Shaban (21) Kocha wa Kichwere FC, mtoto wa tano katika familia ya mzee Shaban, mkazi wa Mtaa wa Bushabani, Kata ya Kibirizi aliiambia Nipashe jinsi alivyotekwa na watu wasiojulikana waliokuwa kwenye gari jeusi.

Anasimulia kuwa akiwa anatokea kwa bibi yake kufunga taa za sola Mtaa wa Buronge, majira ya saa tatu usiku Mei 14, mwaka huu, alikutana na watu asiowafahamu.

Alipofika barabara kubwa ya lami mbele aliliona gari jeusi likiwa limeegeshwa pembezoni, kabla hajalifikia alimulikwa na taa za mwanga mkali wa gari hilo akakosa mwelekeo na kutaka kuanguka ndipo walipotokea watu watatu na kuanza kumshambulia na kumchoma sindano maeneo ya shingoni iliyomfanya kupoteza fahamu.

“Sikujua chochote kilichoendelea mpaka nilipokuja kuamka na kujikuta nipo katika chumba ambacho nilihisi nipo na watu wengine ila sikuweza kuwaona kwa kuwa nilikuwa nimefungwa na kitambaa usoni,” anasema Shaban.

Baadaye alikuja mtu na kumfungua mikono na kitambaa ili atoe nywila kwenye simu yake na kuwapatia namba za baadhi ya ndugu zake na baada ya kufanya hivyo alifungwa tena na kamba na kitambaa usoni.Hakujua kitu kingine kilichoendela baada ya kumpa mtekaji namba za simu za wazazi na ndugu zake mpaka alipojikuta yupo Hospitali ya Rufani ya Mkoa Maweni akipatiwa matibabu na ndugu zake kumwambia alikaa kwa watekaji kwa muda wa siku 11.

Akielezea upatikanaji wa huduma muhimu za kijamii anasema; “Muda wote niliokuwa huko nilijisaidia nilipokuwa nimekaa zaidi haja ndogo, sikupata haja kubwa kwakuwa nilikuwa nikilishwa pumba, unga na maji.”

NDUGU WAELEZA

Akizungumzia tukio hilo kaka yake, Bilali Shaban, anayeshughulika kubeba mizigo katika Mwalo wa Kibirizi, anasema baada ya mdogo wake kutorudi nyumbani mpaka saa tano usiku, walimtafuta kwa kumpigia simu bibi yake.

Bibi yao aliwajibu kuwa kijana huyo alishaondoka muda mrefu, ndipo walipoanza kumtafuta kwa marafiki bila mafanikio. 

"Wasiwasi ulitanda, tulitoka na kuomba msaada kwa majirani ambao walitusaidia kumtafuta, tulianza kwa kutoa taarifa polisi ambao walitushauri kwenda hospitali kwa kuwa saa 24 za kufungua kesi ya kupotea kwa mtu zilikuwa bado ili kufungua jalada, tulifanya hivyo ila hakuwepo huko pia, kwakuwa usiku ulizidi kuwa mwingi tulirudi nyumbani na kusubiri kukuche ili tuendelee na kumtafuta," anasema Bilali.

Juni 15, walitoa tena taarifa ya upotevu wa ndugu yao katika kituo kikuu cha polisi na huko walisema hayupo na kuwataka waende katika kituo cha Kigoma mjini, hata hivyo, hawakufanikiwa kumpata.

"Tulimtafuta siku nzima, kila mahali, lakini hatukumpata, tulikata tamaa na kuwa na maswali mengi kichwani ambayo hayakuwa na majibu, hatukuweza kuwaza mambo mabaya juu yake kwa kuwa Ramadhan si kijana mwenye tabia za ajabu," anasema Bilali.Aidha, anasema saa saba usiku Mei 16, alipigiwa simu na namba mpya, mara tatu, lakini hakupokea kutokana na uchovu, aliziona simu hizo alfajiri saa 10:30 aliposhituka kutoka usingizini zilizoambatana na ujumbe mfupi wa maneno uliosomeka: 

“Mtu wenu mnayemtafuta tunaye sisi, na kama mnamuhitaji itabidi mfuate masharti tutakayowapatia” mnatakiwa mtupatie Sh. milioni 2.5, msipofanya hivyo ndani ya muda tuliowaambia tutamuua na kuchukua figo na maini, maelekezo ya kutuma pesa tutakupatia," ulisema ujumbe huo.

Asubuhi, Mei 17 alifika Kituo Kikuu cha Polisi akiwa na ujumbe na namba ya simu iliyompigia ikihitajika Sh. 50,000 kwa ajili ya ku “track” namba hiyo japo polisi hao hawakurudi na majibu ya uchunguzi wao kwa wahusika mpaka kupatikana kwa ndugu yao licha ya kupewa mwendelezo wa kila taarifa na vitisho walivyokuwa wakivipata kutoka kwa watekaji.

"Tulitoa pesa ya kufuatilia hiyo namba, na tuliendelea kutoa taarifa ya vitisho na taarifa nyingine kutoka kwa watekaji kwa mpelelezi wa kesi tuliyepewa na jeshi la polisi, alituambia tusichukue hatua yoyote, tuliachie jeshi la polisi, lakini kwakuwa vitisho vilikuwa vingi na muda waliotupatia wa kulipa hizo pesa ulikuwa umeisha polisi wakiwa kimya ilibidi tutafute pesa hizo ili kuzituma kupitia namba na maelekezo waliyotupatia," anaeleza Bilali.

"Ilipofika Juni 24, tarehe ambayo watekaji walisema ni siku ya mwisho, asubuhi walipiga simu na kutuambia tuandae matanga kwakuwa ikifika usiku hatujatuma fedha hiyo watamuua Ramadhan, tulikaa kama familia na kuhakikisha fedha imepatikana.

“Tulisubiri watupigie simu wao kwakuwa namba walizokuwa wanatumia kutupigia hazikuwa zikipatikana baada ya kuongea na sisi, na ilipofika usiku walipiga simu na kutupa melekezo ya kutuma hiyo pesa pamoja na ya kutolea, hivyo tulituma Sh. 2,554,000 ilikuwa ngumu sana kwetu kutokana na hali ngumu ya maisha tuliyonayo," anasema Bilali.

Baada ya watekaji kupokea muamala, walipewa maelekezo ya kumpata Ramdhani siku inayofuata, na saa 3:00 usiku Mei 25, mwaka huu, watekaji waliwapigia simu wakiwataka wawe na usafiri kwenda Kijiji cha Msimba eneo lilipo dampo ili wakamchukue ndugu yao, walifanya hivyo na kumkuta akiwa amefungwa kamba miguu na kitambaa machoni.

"Tulimfungua kamba na kuelekea kituo cha polisi cha central ambapo walitupatia PF3, tukampeleka Hospitali ya Rufani ya Maweni, kutokana na hali kuwa mbaya alitundikiwa dripu za chakula, ili apate nguvu pamoja na kupatiwa huduma nyingine muhimu. 

“Tunamshukuru Mungu sasa anaendelea vizuri japo matendo kama haya bado yapo mengi katika jamii na hatujui chanzo chake ni nini,” alisema huku akiliomba jeshi la polisi kuchukua hatua dhidi ya vitendo hivyo vinavyoendelea katika jamii.

WENGINE WALIOTEKWA

Mkazi wa Mwandiga Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma, Lilenga Lilenga (49), anayejishughulisha na shughuli za uvuvi alipotea tangu Mei 11, mwaka huu alipokuwa kwenye shughuli zake mwalo wa Kibirizi.

Akizungumza na mwandishi wa gazeti hili, mke wa Lilenga, Johari Kabwe, anasema sasa ni zaidi ya mwezi mmoja mume wake hajulikani alipo licha ya kutoa taarifa jeshi la polisi ambapo anadai hawawaambii chochote kuhusiana na maendeleo ya kutambua alipo mume wake huku akilitilia shaka jeshi hilo kuhusika na upotevu wa mume wake.

Mama mzazi wa Lilenga, Rehema Mrisho anasema zimefanyika jitihada mbalimbali za kumtafuta ikiwemo kumtangaza kwenye vyombo vya habari na mitandao ya kijamii bila mafanikio. 

Aidha, anaiomba serikali kuingilia kati suala la mtoto wake kupotea ili aweze kurejeshwa, ambaye ni wa pekee anayemlea katika umri wake wa uzee.

Joyce Christant (maarufu mama Rose) mkazi wa Gungu, anakiri kupotea kwa mtoto wake wa kike (20), ambaye hakulitaja jina lake akidai hataki kuzungumza lolote kuhusu tukio hilo kwakuwa hakupata ushirikiano kutoka polisi.

Akisimulia tukio hilo alisema mtoto wake alichukuliwa majira ya saa 2:30 usiku wa Mei 14, 2024 alipokuwa akiuza bidhaa dukani ndipo walifika watu wakihitaji maji ya kunywa na alipowapelekea kwenye gari hakurudi tena.

Mama Rose anasema ili kumpata mwanawe ilibidi afuate maelezo ya watekaji na kulipa Sh.2,500,000 na kisha kurejeshewa mwanawe ambaye tayari alikuwa ameshapelekwa jijini Mwanza.

VIONGOZI SERIKALI WANENA

Mwenyekiti wa Mtaa wa Butunga, Hamis Kalimwagu alithibitisha kuwapo kwa tukio hilo na matukio mengine ambayo yamekuwa yakiendelea kutokea katika mtaa wake yakiwamo kubomoa nyumba, kuiba mifugo na watu kuchomwa visu.

Aidha, aliyahusisha matukio hayo na kusitishwa shughuli za uvuvi katika Ziwa Tanganyika kwa miezi mitatu hali inayosababisha kuwakosesha kipato na kutumia mbinu za utapeli kama wanavyofanya.

Mwenyekiti huyo aliiomba serikali kupunguza miezi ya kufungua ziwa hilo ambalo linategemewa na wananchi hao kujipati kipato.

POLISI 

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma, Philemon Makungu, amethibitisha kuwapo kwa matukio hayo na kusema wanaendelea na uchunguzi kila linaporipotiwa tukio la upotevu.

Amewataka wananchi kutotoa pesa zinazoombwa na watekaji kwa kuwa kitendo hicho kinaweza kuongeza magenge ya kihalifu na badala yake watoe taarifa katika kituo cha polisi ili hatua ziweze kuchukuliwa na watekaji waweze kutiwa mbaroni.

RPC Makungu anasema endapo wananchi watafika vituo vya polisi na kujibiwa vibaya wanapaswa kujua majina ya waliowajibu, ili hatua za kinidhamu ziweze kuchukuliwa dhidi yao kwa sababu wapo kwa ajili ya kusaidia watu na si kuumiza hisia zao.

“Mtu hawezi kuja kituo cha polisi bila sababu za msingi, akijibiwa vibaya akathibitisha muda aliofika na muonekano wa polisi aliyemjibu vibaya kisha atoe taarifa kwa kamanda wa polisi kwakuwa wanaingia kwa zamu ni rahisi kujua nani alikuwapo kwa muda huo ili tumkemee na asirudie,” anasema Makungu.

Aidha, alisema upelelezi wa tukio hilo bado unaendelea.