Wakili: Familia ya wanayemtaja "afande" kushtaki wanaomzushia

By Jenifer Gilla , Nipashe
Published at 10:22 AM Aug 22 2024
Mwanasheria wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Emmanuel Muga.
Picha: Mtandao
Mwanasheria wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Emmanuel Muga.

FAMILIA ya Kamishna Msaidizi wa Polisi (SSP), Fatuma Kigondo, imesema inafikiria kufungua mashtaka dhidi ya waliosambaza kwenye mitandao ya kijamii kuwa ndugu yao amehusika kutuma vijana kumbaka na kumlawiti binti anayedaiwa mkazi wa Yombo Dovya, wilayani Temeke, mkoani Dar es Salaam.

Taarifa iliyotolewa na Mwanasheria wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Emmanuel Muga, kupitia ukurasa wake wa X, ilieleza kuwa ndugu wa Askari polisi huyo waliwasiliana naye na kumweleza kusudio lao hilo, wakiwa na maelezo kuwa wanataka kuhakikisha haki inatendeka na ukweli wa jambo hilo unafichuliwa.

Alisema chanzo cha taarifa hiyo waliyoiita "ya kupotosha" ni mtu anayejitambulisha kama mshawishi wa mitandao ya kijamii na zinasambaa kwa haraka, ikiaminika kuwa ni ya kweli na kuisababisha familia hiyo kukosa amani.

Alisema familia hiyo ilimweleza kuwa SSP Fatuma siyo afande aliyezungumziwa kwenye video yenye utata inayosambazwa kwenye mitandao ya kijamii na kuwa ndugu yao ni ofisa wa polisi mwenye cheo cha SSP na si ASP kama ilivyodaiwa mtandaoni.

"Aidha, familia imethibitisha kuwa SSP Fatuma ni mjane na hana mume ambaye angeweza kuporwa kama ilivyosemwa," alisema.

Kuhusu washukiwa wa ubakaji, alisema familia imesema kuwa wamebainika wanatoka kwenye vikosi vingine visivyo chini ya amri ya SSP Fatuma, hivyo inawapa  maswali kuwa ofisa huyo angewezaje kutoa maagizo kwa washukiwa hao, iwe ni kisheria au isivyo kisheria.

Alisema ndugu hao wamesikitishwa na tuhuma zinazoendelea kwenye mitandao ya kijamii dhidi ya ndugu yao na wangependa kutoa ufafanuzi kuwa hahusiki na madai hayo.

Alisema familia hiyo inasisitiza umuhimu wa umma kuwa na uwazi na kuchunguza kwa kina taarifa zinazozungumzwa kabla ya kuzipokea kama zina ukweli. 

Akizungumza na Nipashe, Wakili Muga alisema, "Familia ya Fatuma wamenitafuta, amelalamika sana, anasema wanamchafua, pia yuko katika hali ya mshtuko na familia yake, hivyo wamenieleza kuwa wanafikiria kuchukua hatua za kisheria." 

Tukio hilo liliibuliwa na aliyekuwa Meya wa Ubungo, Boniface Jacob wiki mbili zilizopita ambaye aliandika mkasa mzima kwenye ukurasa wake wa X huku akiwatumia nakala, Rais Samia Suluhu Hassan kama Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi Tanzania, Waziri wa Ulinzi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Stergomena Tax na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dorothy Gwajima.

Meya Boniface aliandika: "Binti huyu amebakwa na kulawitiwa akiwa anarekodiwa video tatu tofauti. Askari hao walimrekodi wakiwa wanambaka na kumlawiti, wamesambaza video zake mitandaoni kwa maagizo ya kiongozi wao (afande) ambaye amewatuma kumpatia huyu binti adhabu.