Samia atoa motisha kwa wanaohama Ngorongoro

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 07:18 AM Aug 23 2024
Rais Samia Suluhu Hassan.
Picha:Ikulu
Rais Samia Suluhu Hassan.

RAIS Samia Suluhu Hassan, ametoa fedha ya fidia na motisha ya maendelezo yake kwa kila kaya iliyokubali kuhama kwa hiari ndani ya eneo la Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), Sh. milioni 10 ili kupisha shughuli za uhifadhi.

Uamuzi huo wa Rais Samia, unalenga kuwapa hamasa wananchi hao kujenga nyumba nyingine mbadala tofauti na zile za vyumba vitatu wanazopewa na serikali. 

Ofisa Uhifadhi Mkuu na Meneja Mradi wa kuhamisha wananchi kwa hiari, Flora Assey, aliyasema hayo jana katika Wilaya ya Ngorongoro, mkoani Arusha, wakati Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Benedict Wakulyamba akiongoza zoezi la kuwaaga wananchi wengine 367 waliokubali kuhama makazi yao kwa hiari kupisha hifadhi hiyo. 

"Mwitikio wa wananchi wanaoishi ndani ya eneo la Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro kuendelea kuhama kwa hiari unaendelea kwa kasi. 

 Hadi kufikia leo (jana), kaya 79 zenye watu 367 na mifugo 995 zimehama kutoka Ngorongoro kwenda Kijiji cha Msomera, Kata ya Misima, Wilaya ya Handeni na maeneo mengine waliyochagua wenyewe," alisema.

 Awali, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi, Daniel Chegere, alisema NCAA inaendelea kuwaelimisha wananchi umuhimu wa kuhama kwa hiari kwenda maeneo yaliyotengwa na serikali baada ya kujengewa miundombinu ya kisasa yenye huduma muhimu za jamii na usalama zaidi tofauti na ilivyo ndani ya hifadhi hiyo. 

 Chegere, alisema hali ya usalama katika hifadhi hiyo inaendelea vizuri, ulinzi umeimarishwa na wageni wanaotembelea  vivutio wanaendelea na shughuli za utalii bila changamoto. 

Kwa upande wake Wakulyamba, alisema kuondoka kwa kundi hilo ni sehemu ya utekelezaji wa mpango wa kulinusuru eneo la hifadhi hiyo. 

Alisema wananchi wameendelea kuelimishwa na kuhama kwa hiari kwa ajili ya kuboresha maisha yao na kunufaika na fursa za kiuchumi zilizoko nje ya hifadhi. 

Kuanzia Juni mwaka 2022 hadi kufikia mwezi huu, takriban kaya 1,598 zenye watu 9,618 na mifugo 39,779 zimehama ndani ya hifadhi hiyo kwenda Msomera mkoani Tanga na maeneo mengine.