RAIS Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuzindua Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014 Toleo la 2023 jijini Dodoma Februari Mosi mwaka huu yenye lengo la kuleta mageuzi ya utoaji elimu nchini.
Miongoni mwa mageuzi yaliyomo katika sera hiyo ni kufundishwa kwa somo la TEHAMA, mafunzo ya ufundi stadi kuanzia elimu ya msingi na matumizi ya akili unde (AI).
Akizungumza jana jijini hapa, Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa alisema lengo la kufanyiwa mapitio hayo ya sera ni kuwafanya wanafunzi kuwa na umahiri na ujuzi unaoakisi mahitaji kitaifa na kimataifa ili kushindana na kushiriki kikamilifu kwenye soko la ajira duniani.
Alisema sera hiyo itazalisha wanafunzi wenye maarifa, maadili na ujuzi utakaowawezesha wahitimu kwenye ngazi mbalimbali kujiajiri na kuajiri wengine na kuongeza uwezo wa ushindani kwenye soko hilo.
"Mapitio hayo yanaendana na utekelezaji Ilani ya CCM kuhusu kuimarisha huduma za kijamii ambapo imejielekeza kuhakikisha kila rasilimali watu inakuwa na ujuzi," alisema.
Msigwa ambaye ni Katibu Mkuu Wizara, Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, alisema mapitio hayo yameshirikisha wadau na matokeo makubwa yanatarajiwa kwa kuwa huduma ya elimu inagusa jamii moja kwa moja.
"Rais Samia alitangaza na kutoa maelekezo akitaka Wizara ya Elimu ifanye kazi kubwa ya kupitia sera na lengo lilikuwa ni kuwa na sera ambayo itawaandaa wanafunzi kuwa mahiri katika kukabiliana na changamoto za sasa na kujibu mahitaji ya dunia ya sasa," alisema.
Alisema Rais hakupendezwa na wanafunzi kuhitimu shahada huku wakiwa hawana ujuzi katika uzalishaji.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Carolyne Nombo alisema sera hiyo itazinduliwa sambamba na vitendea kazi ikiwamo mkakati wa utekelezaji sera ambao tayari umeandaliwa.
Alisema sera hiyo ilielekeza kuboresha mitaala ya elimu ambayo imeboreshwa kwa ngazi zote kuanzia ngazi ya awali na vyuo vikuu kwa sasa vinaendelea kuboresha.
Alisema mitaala hiyo ni pamoja na wa elimu ya awali, elimu ya msingi kuanzia darasa la kwanza hadi la sita, elimu ya sekondari ngazi ya chini na juu na mafunzo ya ualimu ambayo ilianza kutumika mwaka jana na matunda yameanza kuonekana.
Katibu Mkuu alisema kutokana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia, sekta ya elimu kupitia sera hiyo umeandaliwa mkakati wa matumizi ya TEHAMA katika kujenga uchumi wa kidigitali.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED