Serikali yachunguza udhalilishaji kwenye mikopo ya mtandaoni

By Paul Mabeja , Nipashe
Published at 12:04 PM Jun 28 2024
Mikopo ya mtandaoni.
Picha: Maktaba
Mikopo ya mtandaoni.

SERIKALI imesema Benki Kuu ya Tanzania (BoT) inaendelea na utafiti wa uanzishwaji matumizi ya sarafu za kidijitali za benki kuu (Central Bank Digital Currency).

Vilevile, imetoa ufafanuzi kuhusu mikopo mitandaoni ambayo baadhi ya wakopaji wamekuwa wakidhalilishwa pale wanaposhindwa kurejesha mikopo kwa wakati; watu wao wa karibu kutumiwa ujumbe kuhusu mkopo husika.

Naibu Waziri wa Fedha, Ahmad Chande, amezungumzia mchakato wa sarafu hiyo jana bungeni wakati akijibu swali la Mbunge wa Kigamboni, Dk. Faustine Ndungulile (CCM) aliyetaka kujua mpango wa serikali kuanza matumizi ya sarafu za kidijitali.

Chande amesema BoT imebaini kwamba, kama ilivyo kwa mataifa mengi, uanzishwaji sarafu za kidijitali za benki kuu unahitaji uangalifu na umakini bila kuleta athari hasi katika mifumo ya malipo nchini.

"Na pia kuweza kutatua tatizo halisi la malipo ambapo kwa sasa mifumo iliyopo nchini inakidhi hali halisi ya uwezeshaji mwananchi kutuma fedha na kufanya malipo," amesema.

Amesema soko la nchi bado linahitaji kuendelea kuboreshwa katika kuimarisha mifumo iliyopo kwa kutumia vyanzo vinavyopatikana kwa urahisi na wananchi wengi (simu za kawaida) tofauti na matumizi ya sarafu za kidijitali zinazohitaji matumizi ya simu janja.

"Nchi nyingi ikiwa ni pamoja na majirani zetu na ukanda wetu bado wapo katika hatua hizi za awali za utafiti na kuboresha mifumo ya malipo iliyopo," amesema Chande.

MIKOPO MTANDAONI

Kutokana na majibu hayo, Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson, ametaka kupata ufafanuzi kuhusu kile kinachoendelea mitaani kuhusu mikopo inayotolewa kwa njia ya mtandao na watu kudhalilishwa.

"Sijui kuna mwongozo wowote ama na serikali mmepokea, mnalifanyia kazi ama hilo limekuwaje, maana hata mimi nimepata ujumbe wa mtu akiambiwa sijui anadaiwa.

"Sasa ninawaza mimi ninahusika vipi kwa yeye kudaiwa? Sasa ninaona limelalamikiwa sana na wananchi, sijui mna maelekezo yoyote upande wenu serikali kwa sababu hapa tunazungumzia hayohayo ya fedha za mitandao?" Spika Tulia amehoji.

Ni hoja iliyomwinua Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye, aliyethibitisha kumekuwa na changamoto hiyo.

"Kuna watu ambao wanakopeshana mitandaoni, lakini baadaye wanatumia taarifa za watu wanaomzunguka yule waliyemkopesha kwa maana ya namba za simu na kuanza kumtisha pale ambapo wameshindwa kurudishiwa mkopo wao.

"Hili jambo limetokea kwa wiki kadhaa kama si miezi miwili mitatu na baada ya kuliona tumeagiza wenzetu wa TCRA (Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano nchini), wakishirikiana na Cyber Crime Unit ya Jeshi la Polisi, wanalifanyia kazi.

"Ni matumaini yangu kwamba hii kazi itakamilika mapema ili tuone msingi wa hili jambo, ukubwa wake na wapi wanapozipata hizi namba," amesema.

Nape ameongeza kuwa jambo hilo si la kiungwana na ni kinyume cha sheria na hasa Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi; kutumia taarifa za watu wengine kufanya chochote.