Serikali yawatangazia ‘kiama’ vishoka nyumba za NHC

By Joseph Mwendapole , Nipashe
Published at 09:12 AM Jul 01 2024
Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Ahmed Ahmed (kulia), akiwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii, Tomotheo Mzava, (katikati), na Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Geophrey Pinda, (wa pili kushoto), wakikagua Mradi wa Kawe711.
Picha: Mpigapicha Wetu
Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Ahmed Ahmed (kulia), akiwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii, Tomotheo Mzava, (katikati), na Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Geophrey Pinda, (wa pili kushoto), wakikagua Mradi wa Kawe711.

SERIKALI imeliagiza Shirika la Nyumba (NHC), kufanya msako wa kuwaondoa watu wanaofanya udalali wa nyumba zake kwa kuzichukua na kuwapangisha watu wengine kwa gharama kubwa.

Agizo hilo lilitolewa jana na Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Geofrey Pinda, baada ya Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii, kutembelea miradi ya shirika hilo jijini Dar es Salaam ya Samia Housing Scheme Kawe, Morocco Square na mradi wa 711.

“Nyumba nyingi za NHC zimegeuzwa kuwa mradi wa watu waliokuwa wapangaji wa shirika kwa hiyo nimeiagiza NHC ifanye ukaguzi wa kina kuwabaini watu walioanza kukaa kwenye nyumba hizo na kama ndio wanaoendelea kukaa humo au la,” alisema.

“Na hao ambao wamepewa na waliokuwa wapangaji NHC wajulikane ili waweze kupewa upangaji rasmi badala ya kuwa wanawalipa fedha nyingi watu ambao hawahusiki na nyumba hizi za serikali na nimeambiwa kwamba wanachukua fedha nyingi sana hawa kwa kuwapangisha watu,” alisema.

Pinda alisema baadhi ya watu wamechukua nyumba zaidi ya 10 na kuwapangisha wananchi kwa gharama kubwa hali ambayo alisema serikali haiwezi kuifumbia macho.

Alisema wapangaji lazima walipe kwa wakati kwa kuwa wanapochelewa kulipa pango ndani ya makubaliano ya mkataba na mpangishaji wanasababisha usumbufu.

Kuhusu maendeleo ya miradi hiyo, Pinda alimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuridhia miradi hiyo kuendelea baada ya kusimama muda mrefu kutokana na sababu mbalimbali zilizoelezwa.

Alisema kamati imeridhika kuona majengo mengi yamekamilika na wapangaji wameanza kuingia na wengine kununua nyumba kwenye majengo hayo.

Mkurugenzi wa NHC, Hamad Abdallah alisema mradi wa Samia Housing Scheme wa Kawe wenye nyumba 5,000 unaendelea lakini zote zimeshanunuliwa na wananchi.

Alisema kwa sasa NHC inajipanga kuanza ujenzi wa awamu ya pili ya ujenzi wa nyumba 500 eneo la Kawe na kuongeza kuwa wabunge pia wanajionea maendeleo ya miradi wa nyumba za 711 ambazo ujenzi wake ulisimama kwa miaka mingi.

“Wakati mradi huu unasimama ujenzi ulikuwa ghorofa ya saba, lakini kwa sasa tuko ghorofa ya 12 na ujenzi unaenda kwa kasi na mauzo ya nyumba yameshaanza na ndani ya miezi mitatu tumeshapata shilingi bilioni tatu,” alisema.

Mwenyekiti wa kamati hiyo, Timotheo Mzava, alisema wameridhishwa na maendeleo ya miradi hiyo yote mitatu ambayo kukamilika kwake kutasaidia wananchi wengi kupata makazi nafuu.

“Miradi hii isingefikia hatua hii tunayoona leo kama sio nia ya dhati ya Rais Samia Suluhu Hassan kuwezesha NHC kupata fedha za kuendelea na miradi na sisi tumewaambia kwamba hawana kisingizio tena kwani fedha zimetolewa wafanye kazi,” alisema.

“Hakuna sababu yoyote ya kukwamisha miradi hii kwasababu fedha wameshapewa kwa hiyo sisi tumewasisitiza wasimamie ujenzi huu na hatutaki kuona tena miradi hii inasimama,” alisema Mzava