THRDC kugharamia matibabu ya Sativa

By Pilly Kigome , Nipashe
Published at 05:48 PM Jul 02 2024
news
Picha: Mtandao
THRDC kugharamia matibabu ya Sativa

Mkurugenzi wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania(THRDC), Wakili Onesmo Olengurumwa amesema wanagharamia matibabu ya Edger Mwakalebela (Sativa) aliyefikishwa kupata matibabu katika Hospitali ya Aga Khan ya jijini Dar es Salaam.

Wakili Olengurumwa ameyasema hayo alipokuwa akizungumza na vyombo vya habari katika hospitali hiyo.

Olengurumwa amesema Mwakalebela (Sativa) alitekwa na watu wasiojulikana jijini Dar es Salaam na kumpa mateso makali na baadae kumfyatulia risasi maeneo ya kichwa na risasi hizo zilitokea katika shavu la kushoto la muhanga huyo na watu hao walimtelekeza katika moja ya pori Mkoani Katavi.

Amesema kwa mujibu wa maelezo wa Sativa alipopata fahamu alisota kwa makalio hadi kufikia barabara na kuomba msaada wa magari yapitayo njiani na ndipo lilipofahamika jambo hilo.

Olengurumwa amesema wao kama watetezi wa haki za binadamu walifatilia kwa kina utekaji huo na hawakubaini kosa lolote kutoka kwa muhanga huyo kwani alikuwa ni raia mwema anayeendesha shughuli zake kihalali na ni mwanaharakati wa kawaida.

Hatahivyo wamemuomba Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kuunda Tume maalumu ya kuchunguza sakata hilo kuwakamata wahusika ili kuondoa wanaoichafua na kuitia doa Serikali kwa matukio haya ya utekaji.

“Ikiiundwa tume wanaohusika wachukuliwe hatua maana aliyemuita ni dalali yuko Kimara na gari lililomchukua liligongana na bajaji na bajaji ikaenda kuripo Polisi hivyo wakitafutwa watapatikana” amesema Olengurumwa

Wakili Paul Kisabo (THRDC) amesema hali ya mgonjwa kwa leo angalau inaridhisha kidogo lakini jana askari watano walikuja hospitalini hapo kwaajili yakuchukua maelezo ilishindikana kutokana na hali yake bado ilikuwa si nzuri.

Hata hivyo madaktari wa hospitali hiyo hawakuruhusu kuchukuliwa kwa picha kwa mģonjwa na mahojiano ya aina yoyote kutoka kwao.