Uchaguzi Mitaa wakwaa kigingi

By Romana Mallya , Nipashe
Published at 09:31 AM Aug 22 2024
Mkurugenzi wa Jukwaa la Katiba Tanzania (JUKATA), Bob Wangwe.
Picha:Mtandao
Mkurugenzi wa Jukwaa la Katiba Tanzania (JUKATA), Bob Wangwe.

UCHAGUZI wa Serikali za Mitaa umekwaa kigingi: Mkurugenzi wa Jukwaa la Katiba Tanzania (JUKATA), Bob Wangwe na wenzake wawili wamefungua kesi kupinga mamlaka inayousimamia.

Kesi hiyo imefunguliwa Mahakama Kuu dhidi ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG). 

Bob na wenzake wanapinga uchaguzi wa serikali za vijiji, kamati za mitaa na wenyeviti wa vitongoji kusimamiwa na Ofisi ya Rais - TAMISEMI. 

Kesi hiyo imepokelewa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam na imepangwa kutajwa leo mchana mahakamani huko na itakuwa mbele ya Jaji Wilfred Dyansobera. 

Hivi karibuni, Chama cha ACT-Wazalendo nacho kilitangaza kusudio la kwenda mahakamani kufungua kesi ya kupinga TAMISEMI kusimamia uchaguzi huo ilhali Bunge lilishatoa uamuzi uchaguzi huo usimamiwe na Tume Huru ya Uchaguzi (INEC). 

Azma hiyo ilitangazwa hivi karibuni na Makamu Mwenyekiti wa Taifa wa chama hicho, Tanzania Bara, Is-Haka Mchinjita, wakati akizungumza na wananchi jijini Tanga katika mkutano wa hadhara. 

"Niwaambie ACT-Wazalendo tunajiandaa kufungua kesi wiki hii, tunaipeleka TAMISEMI mahakamani kuishtaki kwa kuwa wana nia ya kusimamia uchaguzi wakati kuna uamuzi wa Bunge ukielekeza INEC," alisema.

 Julai 25 mwaka huu, katika ukurasa wake wa X, Katibu Mkuu wa CHADEMA, John Mnyika, pia aliandika: “…hatua zinazohitajika ni zilezile mbili baada ya waziri kutunga kanuni za uchaguzi ambazo ameanza kuzitumia: 

 "Mosi, kanuni hizo zipingwe mahakamani ili TAMISEMI izuiwe kusimamia uchaguzi badala yake, usimamiwe na Tume Huru ya Uchaguzi.

 "Pili, maandalizi yaendelee katika kila mtaa, kijiji na kitongoji kukabiliana na wezi wa kura kwa nguvu ya umma."

 Agosti 16 mwaka huu, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais - TAMISEMI, Mohamed Mchengerwa, alitangaza tarehe rasmi ya uchaguzi huo kuwa ni Novemba 27 mwaka huu.

 Vyama 18 kati ya 19 vyenye usajili wa kudumu nchini vilihudhuria tukio hilo la kutangazwa tarehe ya uchaguzi huo. CHADEMA haikupeleka mwakilishi katika tukio hilo.

 Uongozi wa chama hicho ulisema haukushiriki tukio hilo kutokana na barua kuwafikia wakati Mwenyekiti wao Taifa, Freeman Mbowe na viongozi wengine waandamizi walikuwa wanashikiliwa na Jeshi la Polisi.