Vyombo vya moto ambavyo havijakaguliwa mwisho Agosti 26 kutembea barabarani

By Paul Mabeja , Nipashe
Published at 01:14 PM Aug 22 2024
Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani nchini Ramadhan Ng'azi.
Picha: Paul Mabeja
Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani nchini Ramadhan Ng'azi.

MKUU wa Kikosi cha Usalama Barabarani nchini Ramadhan Ng'azi amesema baada ya Agosti 26 mwaka huu vyombo vyote vya moto ambavyo havijakaguliwa havitaruhusiwa kutembea barabarani.

Ng'azi amebainisha hayo leo Agosti 22 wakati akizungumza na wandishi wa habari kuhusu maadhimisho ya Wiki ya nenda kwa Usalama Barabarani na maadhimisho ya miaka 50 ya Baraza la Taifa la Usalama Barabarani, yatakayofanyika Agosti 26 mwaka jiji Dodoma.

Amesema, vyombo vyote vya moto nchini ambavyo havitakaguliwa kwa hiyali hadi kufikia siku hiyo havitaruhusiwa kutembea barabarani.

"Vyombo vyote vya moto nchini ambavyo havitafanyiwa ukaguzi havitaruhusiwa kutembea barabarani hadi vikaguliwe na kupatiwa stika.

"Chombo ambacho kitakamatwa barabarani kikiwa hakijakaguliwa kitakamatwa na kupelekwa polisi kwa ajili ya ukaguzi na kama kitakaguliwa na kukutwa kikiwa bado na matatizo kitarudishwa tena hadi kionekane kuwa kipo sawa kwa ajili ya matumizi ya barabara zetu" amesema Ng'azi

Aidha, amewataka wamiliki wa vyombo vya moto nchini kutumia kipondi hichi kukaguliwa kwa hiyali na kupatiwa stika ambazo zinaonyesha kuwa chombo hicho kiko salama kutembea barabarani.

"Nitoe wito kwa wamiliki wa vyombo vya moto nchini kutumia kipindi hichi kilichobaki kufanya ukaguzi wa vyombo vyao ili kuepusha usumbufu wa kukamatwa na jeshi la polisi wakati wa ukaguzi"amesema

Akizungumzia kuhusu mabasi yanayotembea usiku amesema kikosi cha usalama barabarani kimeweka mikakati ya kuzuia ajali ikiwemo kupima kiwango cha ulevi cha madereva.

Amesema,mikakati mingine ni kuhakikisha wanafunga vifaa vya kudhibiti mwendo kasi pamoja na mabasi yanayosafiri umbali mrefu kuwa na madereva wawili.

Naibu Kamishna wa Jeshi la Polisi mstaafu, Mohammed Mpinga amesema katika maadhimisho ya wiki hiyo pamoja na mambo mengine utazinduliwa mkakati wa kukabiliana na ajali nchini.

"Mwaka huu pamoja na maadhimisho ya wiki ya nenda kwa usalama barabarani pia ni maadhimisho ya miaka 50 baraza la taifa la usalama barabarani hivyo mkakati mwingine wa kukabiliana na ajali utazinduliwa kwa ajili ya miaka mingine 50" amesema

Pia, amesema katika wiki ya usalama barabarani mwaka huu mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Makamu wa Rais Dk.Philip Mpango ambapo baadhi ya shughuli zitakazofanyika ni pamoja na utoaji elimu kwa wananchi juu ya masuala ya usalama barabarani.

Hata hivyo, amesema jukumu la usalama barabarani ni la kila mtu hivyo wanachi wanapaswa kujitokeza kwa wiki wakati wa maadhimisho hayo ili kupata elimu mbalimbali kuhusu masuala ya usalama barabarani.