Wafungwa, mahabusu kuwekewa vituo vya uandikishaji wapigakura

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 11:04 AM Feb 02 2025
Mkurugenzi wa Uchaguzi wa INEC, Ramadhani Kailima
Picha: Mtandao
Mkurugenzi wa Uchaguzi wa INEC, Ramadhani Kailima

TUME Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) kwa mara ya kwanza inaanza uandikishaji wapigakura kwa wafungwa, wanafunzi wa vyuo vya mafunzo na mahabusu kwa kuweka vituo kwenye magereza yote Tanzania Bara na Zanzibar.

TUME Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) kwa mara ya kwanza inaanza  uandikishaji wapigakura kwa wafungwa, wanafunzi wa vyuo vya mafunzo na mahabusu kwa kuweka vituo kwenye magereza yote Tanzania Bara na Zanzibar.

Takriban vituo vya uandikishaji 130 vinatarajiwa kuwekwa kwenye magereza ya Tanzania Bara na 10 upande wa Zanzibar.

Mkurugenzi wa Uchaguzi wa INEC, Ramadhani Kailima, alisema jana alipokuwa akitoa mada kuhusu maandalizi ya uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapigakura awamu ya kwanza kwa wadau wa uchaguzi mkoani Tanga. 

Kailima alisema kanuni ya 15(2)(C) ya Kanuni za Uboreshaji wa Daftari, Tume imeweka utaratibu wa kuwezesha wafungwa, wanafunzi wa kifungo cha chini ya miezi sita na mahabusu kuandikishwa kuwa wapigakura.

“Hatua hii ni kwa mara ya kwanza kufanyika hapa nchini, hivyo niliombe Jeshi la Magereza kutoa ushirikiano pale shughuli husika itakapoanza kufanyika kwenye maeneo hayo,” alisema.

Hata hivyo, alisema kwa kuzingatia matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya  Mwaka 2022, katika mkoa wa Tanga, tume inatarajia kuandikisha wapigakura wapya  244,805 ikiwa ni ongezeko la asilimia 18.7 ya wapigakura walioko kwenye Daftari la Kudumu la Wapigakura 1,304,235.

Kwa mantiki hiyo,  kwa mkoa wa Tanga, tume inatarajia kukamilisha zoezi la uandikishaji kwa wapigakura wapatao 1,549,040.

Akifungua mkutano huo, Mwenyekiti wa INEC, Jaji Jacobs Mwambegele, alisema lengo la kikao hicho ni kupeana taarifa kuhusu hatua mbalimbali zinazochukuliwa na Tume ili kufanikisha zoezi la uboreshaji wa Daftarai la Kudumu la Wapigakura.

Jaji Mwambegele alisema utekelezaji huo ni takwa la Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani Na. 1 ya mwaka 2024 kifungu cha 16(5) kinachoweka sharti kwa tume kuboresha Daftari la Kudumu la Wapigakura mara mbili kati ya uchaguzi mkuu uliomalizika na kabla ya siku ya uteuzi wa wagombea kwa ajili ya uchaguzi mkuu unaofuata.

Alisema mpaka sasa takribani mikoa 25 nchini imeshakamilisha uboreshaji na mchakato huo unaendelea kwa mikoa iliyobaki kwa upande wa Tanzania Bara na Zanzibar.

“Kwa hapa Tanga kazi itafanyika kwa siku saba kuanzia Februari 13 hadi Februari 19, mwaka huu,  na vituo vitafunguliwa saa 2:00  asubuhi mpaka 12:00 jioni, hivyo tuhamasishe wananchi kujitokeza kuboresha taarifa zao,” alisisitiza.

Jaji Mwambegele alisema katika kuhakikisha tume inakwenda sambamba na mabadiliko ya teknolojia, imeboresha mfumo wa uandikishaji ambapo mpigakura aliyepo katika daftari, ataboresha taarifa zake kwa kutumia aina yoyote ya simu ya kiganjani au kompyuta.

“Wanaotumia simu hata kitochi au kiswaswadu wanaweza kutumia namba *152*00# kisha namba 8 na kisha namba 2 halafu 3 na wataendelea na maelekezo kwa simu husika,” alisema.

Wapigakura 4,369,531 wanatarajiwa kuboresha taarifa zao ambapo 594,494 wanatarajiwa kuondolewa kwenye daftari kwa kukosa sifa za kuendelea kuwapo kwenye daftari, hivyo baada ya uboreshaji, daftari linatarajiwa kuwa na jumla ya wapigakura 34,746,638.