Watanzania milioni sita hatarini kupata upofu

By Faustine Feliciane , Nipashe
Published at 07:56 PM Jul 01 2024
Afisa Mtendaji Mkuu wa Tigo, Kamal Okba (kushoto) akimkabidhi mwenyekiti wa taasisi ya KSI Charitable Eyes Center, Anvelari Rajpar mfano wa hundi ya zaidi ya shilingi milioni mitatu zitakazosaidia kutoa huduma ya matibabu ya macho.
Picha: Mpigapicha Wetu
Afisa Mtendaji Mkuu wa Tigo, Kamal Okba (kushoto) akimkabidhi mwenyekiti wa taasisi ya KSI Charitable Eyes Center, Anvelari Rajpar mfano wa hundi ya zaidi ya shilingi milioni mitatu zitakazosaidia kutoa huduma ya matibabu ya macho.

WATANZANIA milioni sita wapo hatarini kupata upofu wa kudumu kutokana na kushindwa kupata huduma ya upasuaji wa mtoto wa jicho kwa wakati kutokana na sababu mbalimbali.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu akizundua kituo cha hisani cha matibabu ya macho cha K.S.I jijini Dar es Salaam.

Amesema kwa mujibu wa takwimu ya Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa (WHO) zinaeleza kwa Tanzania, watu milioni 12 hawana uhakika wa kupata huduma sahihi ya macho hususani maeneo ya vijijini.

“Hii inaonyesha bado hatujawafikia watanzania wengi katika kuwapa huduma za macho, lakini pia takwimu hizo zinaeleza kati ya watu hao milioni 12, watu milioni sita wapo hatarini kupata upofu wa kudumu kwa kukosa matibabu ya haraka ya upasuaji wa mtoto wa jicho,” amesema Waziri Ummy.

Aidha, amesema juhudi zaidi zinatakiwa katika kufikisha huduma hizo vijijini pamoja na kutoa elimu kwa wananchi umuhimu wa kuwahi kupata huduma ya macho ikiwa pamoja na upasuaji wa mtoto wa jicho.

Amesema sababu nyingine inayotishia kuwapo kwa idadi hiyo ya watu wanaoweza kupata upofu wa kudumu, ni imani potofu juu ya upasuaji wa mtoto wa jicho.

“Baadhi ya maeneo hapa nchini kumekuwa na imani potofu kwa baadhi ya wananchi juu ya upasuaji wa mtoto wa jicho, wapo wanaosema ukikubali kwenda kufanyiwa upasuaji unakuwa kipofu, hii si kweli na lazima elimu itolewe kwa watu kujua umuhimu wa kuwahi matibabu hasa ya mtoto wa jicho,” amesema Ummy.