Watu 20,000 watibiwa bure Arusha, wazidi kufurika kupata matibabu

By Beatrice Shayo , Nipashe
Published at 06:43 PM Jun 28 2024
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda, akizungumza na wananchi waliojitokeza kupatiwa huduma ya matibabu ya bure.

ZAIDI ya wagonjwa 20,000 wametibiwa kwa siku nne katika kambi ya matibabu inayoendelea mkoani Arusha na wengine kupatiwa rufani kwa ajili uchunguzi zaidi katika hospitali mbalimbali nchini.

Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda, ameyasema hayo leo wakati akizungumza na wananchi waliojitokeza katika kambi ya matibabu bure kwenye viwanja vya michezo vya Sheikh Amri Abeid jijini Dar es Salaam.

Amesema idadi hiyo ni kubwa ya waliotibiwa ambao ni wananchi walikuwa wanaishi nyumbani wakiwa wamekata tamaa, hawana fedha ya kumuona daktari, kununua dawa na kufanya vipimo.

“Walijikatia tamaa na kumuomba Mungu wao bahati nzuri amewasikia kilio chao na ndio maana tunashukuru kwa idadi hiyo kubwa na watu wamezidi kuongezeka tayari tumeongeza idadi ya madaktari na dawa,”amesema Makonda.

Amesema tayari wameunda kamati ya rufaa wapo wanaopimwa na kupatiwa dawa na wengine wanapelekwa hospitali nyingine kwa ajili ya upasuaji.

“Ombi langu tuwe na uvumilivu ukiambiwa uende hospitali ya Mount Meru sio kwamba ukifika tu unafanyiwa upasuaji zipo taratibu za kufanyiwa upasuaji sio ukifika tu unaanza kusema nimeambiwa nikifika nafanyiwa upasuaji fuata taratibu hakuna ambaye ataachwa bila kupatiwa matibabu,”amesema Makonda.

Makonda alisema lengo lao ni kuhakikisha kila mmoja anapatiwa matibabu na kurejea katika afya yake, hivyo ni muhimu kwa kila mmoja kufuata maelekezo wanayopatiwa.