KAMPENI za uchaguzi wa serikali za mitaa, zinaanza kesho hadi Jumanne ijayo Novemba 26. Ni muda kwa wagombea wa vyama mbalimbali vya siasa kumwaga sera na kile walichotumwa na vyama vyao kukitangaza majukwaani.
Wakati kampeni zinaanza, wanawake 12 kutoka baadhi ya kata za Dar es Salaam, wamepata Sh. milioni 1.2 kwa ajili ya kuendeshea kampeni hizo zitakazodumu kwa wiki moja.
Wanawake hao wanawania ujumbe wa serikali za mitaa katika kata za Mzinga, Kivule na Kipunguni wakinufaika na fedha zilizochangwa na kinamama 70 ambao ni wajasiriamali wadogo.
Kila mmoja katika michango hiyo, alikuwa akitoa Shilingi 200 kila siku kwa miezi minne, kazi inayoratibiwa na Kituo cha Sauti ya Jamii Kipunguni kuwezesha wanawake kutoka vyama mbalimbali vya siasa wanaoshiriki uchaguzi kunufaika.
Mkurugenzi wa kituo hicho, Seleman Bishagazi, analiambia gazeti hilo kuwa wagombea 12, kila mmoja amepewa Sh.100,000 za kampeni ili angalau kuwapunguzia makali kwenye jukumu hilo.
Akifafanua jinsi michango hiyo ilivyoanza, anasema moja ya majukumu yao ni kuhamasisha wanawake wajitokeze kwa wingi kuingia katika uongozi kwa kuwa mchango wao unahitajika kubadilisha na kuboresha maisha na kufikia maendeleo.
"Lakini moja ya changamoto ambayo wamekuwa wakisema licha ya kwamba wanaonekana wana uwezo wa kuongoza, ni ukosefu wa fedha za kufanikisha kampeni," anasema Bishagazi.
Anatoa mfano kuwa mgombea anaweza kupitishwa na chama chake, akateuliwa kuwani uongozi na kwamba chama chake kinaweza kumwambia agharamie kampeni lakini hana fedha.
"Kwa ujumla fedha zinahitajika kwa vitu mbalimbali katika kampeni, lakini kinamama wengi wanakwama kutokana na ukosefu wa fedha. Baada ya kubaini hilo tukaanzisha mkakati huu," anasema.
Anafafanua kuwa waliamua kuuanzisha kuwezesha wanawake wenye nia ya kugombea kwa kushirikisha wajasiriamali wanawake ambao wamefanikisha fedha hizo.
Bishagazi anasema wanawake 12 waliowezeshwe na wajasiriamali wenzao ni kutoka vyama vya CCM na CHADEMA ambao tayari wamekabidhiwa kitita tayari kwa kampeni.
"Ninajua kiasi cha fedha walichopewa siyo kingi, lakini angalau kwa mwanzo huu, ujumbe wetu wa kutaka kuinua wanawake wengi ili waingie wengi katika ngazi za maamuzi umefanikiwa," anasema.
NENO LA WANUFAIKA
Rehema Mfaume anayewania ujumbe wa serikali ya mtaa Kivule kwa tiketi ya CHADEMA, anasema hatua ya baadhi ya wajasiriamali hao kuchanga Shilingi 200 kila mmoja ili kusaidia kinamama wagombea bila kujali vyama kinaonyesha mshikamano.
"Mara nyingi kumekuwa na dhana kwamba wanawake hawapendani, lakini kitendo hiki cha wauza mihogo ya kukaanga, miguu ya kuku na vitu vingine vidogo kutuchangia fedha za kampeni, kimeonyesha mshikamano ambao kinamama tunao," anasema Rehema.
Aidha, mara nyingi watu wamekuwa wakichangishana fedha kwa ajili ya harusi na sherehe mbalimbali, lakini kwa Kituo cha Sauti ya Jamii Kipunguni imekuwa ni kinyume kwa kuhamasisha fedha kwa maendeleo, anasema.
"Mkakati wa aina ufike Tanzania nzima ili katika uchaguzi mkuu, wanawake watakaojitokeza kuwania udiwani, ubunge na hata urais, wapigwe tafu kwa ajili ya kufanikisha kampeni," anasema.
Mnufaika mwingine wa Sh. 100,000 Mwanahamisi Kassim kutoka Kata ya Mzinga anayewania ujumbe wa serikali mtaa kupitia CCM, anasema kilichofanywa na wanawake wajasiriamali ni cha kuigwa.
"Wanawake bado tunahitaji kuongezewa nguvu ili tuweze kuwa wengi katika uongozi ili tulingane na idadi ya wanaume. Hivyo, hiki ambacho kimeanzishwa na wenzetu si haba," anasema Mwanahamisi.
Mwanahamisi anasema kuna umuhimu mkubwa kumuunga mkono mwanamke katika uongozi, kwa maelezo kuwa naye ana nafasi yake kwa maendeleo jamii na taifa kwa ujumla.
Happy Mhagama naye amejitosa kuwania ujumbe wa serikali ya Mtaa wa Machimbo Kata ya Kipunguni kwa mara ya tatu kupitia CCM, anasema amevutiwa na mkakati wa wanawake wenzake kuchanga fedha hizo.
UCHAGUZI 2019
Monica John Ofisa ni Habari wa Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), anasema kwa mujibu wa takwimu za uchaguzi wa serikali za mitaa ya mwaka 2019 asilimia 2.1 ya wenyeviti wa vijiji wanawake.
Ofisa habari huyo amewahi kusema hayo katika mafunzo ya waandishi wa habari kutoka mikoa ya Mtwara, Lindi, Pwani na Dar es Salaam yalifanyika jijini Dar es Salaam, kwamba takwimu hizo haziridhishi katika kuzingatia usawa wa kijinsia.
Kutokana na hali hiyo, anawahimiza waandishi wa habari kuandika habari zenye mlengo wa kijinsi, hasa katika kuhamasisha ushiriki wa wanawake wajitokeze kuwania nafasi mbalimbali za uongozi.
"Kutokuwa na viongozi wanawake kuanzia ngazi za maamuzi na serikali za mitaa mambo mengi ya kijinsia yatakuwa yanasahaulika katika sera, mipango, bajeti na nyenzo mbalimbali ambazo zinasaidia kuleta maendeleo katika taifa letu," anasema Monica.
Anasema zipo changamoto mbalimbali ambazo wanawake zinawakabili katika michakato ya uchaguzi kuanzia kwenye kuchukua fomu hadi kwenda kwenye kampeni.
"Zamani kulikuwa na ile hali kwamba wanawake hawapendani au hawawezi akamchagua mwanamke mwenzao. Huo ni mtazamo potofu lakini kuna mahali wapo wanawake wanamwamini mwanamke mwenzao, kwa hiyo waandishi wa habari hampaswi kuchukua mtazamo hasi, badala yake mhamasishe mtazamo chanya ili wengine waamke," anasema.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED