MKUTANO wa 19 wa kilele wa kundi la nchi tajiri na zile zinazoendelea kiuchumi la G20 unafanyika jijini Rio De Jenairo, Brazil ambapo ushiriki wa Tanzania unatajwa kufanikisha kushawishi kupata fedha za masharti nafuu na ushirikiano kwa ajili ya kupanua kampeni ya upatikanaji wa nishati safi.
Rais Samia Suluhu Hassan ni miongoni mwa marais wanaoshiriki mkutano huo wa siku mbili, akihudhuria kwa mara ya kwanza, akiwa mkuu wa nchi mwanamama kutoka Afrika.
G20 ni jukwaa la kimataifa linalojumuisha nchi wanachama 19 pamoja na Umoja wa Ulaya na Umoja wa Afrika (AU).
Umoja wa Afrika unashiriki kwa mara ya kwanza katika mkutano huo kama mwanachama baada ya kukubaliwa Septemba 2023.
Kualikwa kwa Rais wa Tanzania Samia ni heshima kwa taifa kupata fursa hiyo ambayo inaifanya nchi kuaminika kwenye jumuiya ya kimataifa.
Mageuzi makubwa ya kiuchumi yaliyofanywa na Rais Samia na kampeni yake ya matumizi ya nishati safi yamewavutia viongozi wengi duniani kiasi cha kuamua awe mmoja wa washiriki wa mkutano huo ambao hufanyika mara moja kila mwaka.
Mbali na kujadili masuala yanayohusu maendeleo ya mataifa yao nchi hizo zilizoendelea na tajiri pia zimekuwa zikitoa maazimio mbalimbali ya kuzikwamua nchi zinazoendelea kutoka kwenye umaskini.
Hivyo kwa Tanzania kuwa miongoni mwa waalikwa kwenye mkutano huo ni jambo la kujivunia ambalo linaipa heshima nchi kwenye uso wa dunia kuonekana kama moja ya nchi zinazofanya vizuri kwenye nyanja ya uchumi.
Katika mkutano wa viongozi wa G20 ambao ulifanyika 2023 huko New Delhi India ulikuwa na kauli mbiu ya 'Dunia Moja, Familia Moja na Mustakabali Mmoja.
Katika tamko lililopitishwa katika mkutano huo wa mwaka jana, viongozi wa G20 walitoa ahadi za kuharakisha utekelezaji wa ajenda ya 2030 ya Maendeleo Endelevu, kukabiliana na maendeleo na changamoto za hali ya hewa.
Ahadi nyingine ya viongozi wa G20 nchini India ilikuwa kuongeza uwezo wa nchi zinazoendelea kukabiliana na dharura za kiafya na kushughulikia udhaifu uliopo kwenye ulipaji wa madeni ya nchi zinazoendelea.
Maazimio mengine yalikuwa ni kukuza benki za maendeleo za mataifa mengi yanayoendelea, kukuza usawa wa kijinsia, kuimarisha sauti ya nchi zinazoendelea katika maamuzi ya kimataifa.
Hivyo macho na masikio ya mataifa yanayoendelea ni Rio Dijaneiro Brazil kusikia maazimio ya New Delh ya mwaka jana yalitekelezwa kwa kiwango gani na je wameazimia nini kusaidia nchi zinazoendelea kwenye mkutano wa mwaka huu.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mahmoud Thabit Kombo, anasema Tanzania imepewa nafasi adhimu ya kukaa mezani na kundi ambalo linashikilia asilimia 75 ya biashara ya kimataifa na asilimia 85 ya pato la dunia.
“Huu ni ushuhuda wa kazi ya Rais wetu bila kuchoka katika azma yake ya kutoa njia za kuhamisha teknolojia na msaada wa kifedha kwa Tanzania na nchi nyingine za Afrika,” anasema katika taarifa yake.
Anaongeza kuwa ushiriki wa Tanzania katika mkutano huo utasaidia juhudi za serikali katika mapambano dhidi ya umaskini na njaa na kufikia malengo ya maendeleo endelevu.
Waziri Kombo anasema ushiriki wa Rais Samia pia utaongeza mipango ya upishi safi na miundombinu mbadala muhimu kwa maisha endelevu.
Anaongeza kuwa mkutano huo utaipa Tanzania fursa ya kuvutia uwekezaji katika mipango ya usalama wa chakula kwa kukuza kilimo kinachozingatia hali ya hewa, kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi hususan kwenye mifumo ya chakula na kuimarisha ustahimilivu wa kikanda.
Waziri anasema ushiriki wa Rais Samia katika mkutano wa G20 unatarajiwa kuinua hadhi ya Watanzania katika ngazi ya dunia ili kukuza ushirikiano wa muda mrefu katika kufikia dira ya muda mrefu inayoendana na malengo ya maendeleo.
Anasema mkutano wa viongozi wa G20 utajadili vipaumbele vya maendeleo endelevu ambavyo ni ushirikishwaji wa kijamii na mapambano dhidi ya njaa na umaskini, mabadiliko ya nishati sambamba na kukuza maendeleo endelevu katika nyanja zote za kiuchumi, kijamii na kimazingira.
G20 inaundwa na Argentina, Australia, Brazili, Canada, China, Ufaransa, Ujerumani, India, Indonesia, Italia, Japan, Mexico, Urusi, Saudi Arabia, Afrika Kusini, Korea Kusini, Uturuki, Uingereza na Marekani.
Kundi hilo linaangalia ukuaji wa uchumi duniani, kushughulikia masuala muhimu ya kimataifa kama vile mabadiliko ya hali ya hewa, usalama wa nishati na maendeleo, na kukuza ushirikiano wa kimataifa katika masuala muhimu kama vile biashara, fedha na uwekezaji.
Mkutano wa 18 wa G20 mwaka 2023 ulifanyika New Delh India.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED