Wabunge Viti Maalum wakumbushwa 2025 kuhamia nafasi za majimboni

By Rahma Suleiman , Nipashe
Published at 09:07 AM Nov 20 2024

Wawakilishi wa viti maalum wakiwa kwenye kikao cha Baraza la Wawakilishi Chukwani Zanzibar, kutoka kushoto ni Zainab Abdallah Salum, Mwanaidi Kassim na Salma Mussa Bilali.
PICHA: RAHMA SULEIMANI
Wawakilishi wa viti maalum wakiwa kwenye kikao cha Baraza la Wawakilishi Chukwani Zanzibar, kutoka kushoto ni Zainab Abdallah Salum, Mwanaidi Kassim na Salma Mussa Bilali.

ZANZIBAR ina safari ndefu kufikia azma ya azimio la Maputo linaloangazia uwakilishi wa usawa wa kijinsia wa uwiano wa 50/50 barani Afrika kwenye medani za kisiasa na uongozi wa umma.

Idadi ya wawakilishi wanawake wakuchaguliwa katika majimbo kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 si kubwa hivyo wanahitaji waongezeke.

Kwa mujibu wa takwimu za baraza la wawakilishi lina wajumbe 78 kati ya hao wanawake 29 na wanaume 48.

Kwenye idadi hiyo, wanawake  wawakilishi kutoka uchaguzi mkuu  majimboni ni nane na wakati wanaume ni 42, wanawake wa viti maalum 18 na wajumbe wa kuteuliwa na rais wanane.

Mwaka 2025 ni uchaguzi mkuu, hivyo ni vyema idadi ya wanawake ikaongezeka katika nafasi za uongozi ikiwamo udiwani, uwakilishi na ubunge wa kuchaguliwa majimboni badala ya wanawake kutegemea viti maalum.

Na huo ndiyo wakati ni huu kwa wabunge, wawakilishi na madiwani kupitia viti maalum wanawake, watoke na kuungana na wanawake wengine kuwania katika majimbo ya uchaguzi.

Wafike huko kupambana na yeyote kwa kuwa tayari wameshapata uzoefu wa kutosha hivyo kuwapa nafasi wanawake wengine washike nafasi zao.

Uwalikishi wa wanawake kupitia viti maalum si uwakilishi wa kudumu bali ni nafasi za kujiandaa kisiasa, kujipima lakini pia za kupata uzoefu na kutumikia wananchi.

Kwa kuwa wawakilishi na wabunge wa viti maalum wameshapata mwanga, upeo na maarifa ya kazi hizo, hivi sasa yatosha waende na kwenda kuchuana kwenye majimbo ya uchaguzi.

Wapo ambao wamekaa kwenye nafasi hizo kwa miaka mitano, 10 na wengine hadi vipindi vinne. Wawakilishi, wabunge na madiwani hao wajiondoe na kwenda majimboni.

Kila mtu anajua kuwa licha ya kupata uzoefu, maarifa na ujuzi wa kisiasa, wameshajua mbinu za kupata ushindi na jinsi walivyojijenga katika jamii.

Mahusiano, ushirikiano na maelewano yao katika majimbo, kati ya wananchi yatakuwa yameimarika sana hivyo ni wazi watakuwa na ubavu wa kuwania nafasi katika majimbo ifikapo 2025.

Mwanahamis Kassim ambaye sasa ndiye mbunge wa jimbo la Magomeni Zanzibar, amewahi kuwa mbunge wa viti maalum kwa miaka mitano bungeni, ameamua kuwania uongozi jimboni na kushinda katika uchaguzi wa mwaka 2020.

Uthubutu na uwezo wake umemfanya kupambana na kuwashinda wanaume waliokuwa wakipambana naye kwenye nafasi hiyo lakini kura zilimiminikia  na kulitwaa jimbo hilo.

Kwa mfano huo na mengine kuna wabunge, wawakilishi na madiwani kadhaa ambao kutokana na kuchapakazi  katika kutumikia nafasi hizo, tunaamini wakiamua kwenda majimboni lazima washinde.

VING’ANG’ANIZI 

Sababu za kung’ang’ania viti maalum, zinatajwa na mwakilishi wa jimbo la Kiwengwa, Asha Abdallah Mussa, anayesema umefika wakati sasa wa wanawake kujikita majimboni kuwania uongozi badala ya kutegemea viti maalum.

Anasema hofu, woga, kutojiamini na mifumo dume ndiyo inayosababisha wanawake wengi kugombea nafasi za uongozi majimboni na nafasi hizo kuwaachia wanaume.

“Si kwamba wanawake hatuwezi kupambana na wanaume kugombea nafasi za uongozi majimboni, ni woga na hofu tu tuliyokuwa nayo. Tuwe na uthubutu wa kugombea majimboni ili kuwa na uwiano katika vyombo vya maamuzi,” anasema.

Anasema wanawake wengi wakati wa uchaguzi mkuu hujikita hasa kwenye viti maalum kuliko nafasi za majimbo kwa sababu kwenye majimbo huwaogopa wanaume katika kushindana nao.

“Ukiangalia majimboni wapiga kura wengi ni wanawake lakini changamoto iliyopo ni mifumo dume. Yapo baadhi ya maeneo mifumo dume hiyo imeanza kuondoka na nafasi katika vyombo vya maamuzi ikiwemo baraza la wawakilishi imeongezeka kwa wanawake waliochaguliwa majimboni ikilinganishwa na miaka iliyopita,” anasema.

Asha ambaye ni mwanamke wa kwanza kwa nafasi ya uwakilishi katika jimbo la Kiwengwa, anasema wanawake wapiga kura majimboni wana imani na wanawake katika kuwaongoza.

“Hata wanaume waliopo majimboni wanatuamini wanawake, na tunasema wanawake hatutarudi nyuma na wakati ukifika tutakwenda kupambana nao kuchukua fomu kugombea nafasi za uongozi majimboni kushiriki uchaguzi mkuu 2025.”

Mwakilishi wa jimbo la Fuoni, Yussuf Hassan Iddi, anasema tatizo kubwa la wanawake kung’angania viti maalum kuliko kwenda majimboni, wanahisi kama kuna ugumu fulani majimboni.

Anasema ni suala la uthubutu hakuna ugumu kwa sababu wakijaribu wanaweza na wapo wawakilishi na wabunge wanawake ambao wanahudumia katika majimbo ya uchaguzi.

“Kwa mfano katika majimbo yuko Mtumwa Peya jimbo la Bubwini, Asha Abdallah Mussa  Kiwengwa na wengine na hawa ukiwauliza vipi unaweza kwenda viti maalum kugombea watakuambia hawawezi maana huko nako kuna changamoto zake na wameshazowea majimboni,” anasema mwakilishi huyo.

Aidha, anasema kuna changamoto kati ya wanawake wenyewe, kushindwa kuungana mkono hasa ikizingatiwa kuwa katika majimbo ya uchaguzi asilimia kubwa ya wapiga kura ni wanawake, hivyo anapotokezea mgombea mwanamke kumuunga mkono ili kufikia asilimia 50 kwa 50 katika vyombo vya maamuzi ikiwemo Bunge na Baraza la Wawakilishi.

Mwakilishi huyo anasema ni jambo jema kuwepo kwa kanuni nafasi za viti maalumu kuhudumu kwa muda wa vipindi viwili tu, ili kuwapisha wengine kupata uzoefu na kujengewa uwezo na wale ambao wameshahudumu vipindi viwili kwenda majimboni kugombea.

Anasema licha ya kwamba jimboni kuna changamoto nyingi ambapo kwa mwanamke zinaweza kumletea shida ikiwemo mfumo dume ambao unawarejesha nyuma wanawake kuingia majimboni kugombea.

Anautaja woga na kutojiamini, hivyo ni vyema kujiamini na kuondosha woga na wakiingia majimboni wana uwezo wa kushinda.

“Mimi sina wasiwasi na wanawake ikifika muda wa kugombea kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa 2025 wanawake waje katika Jimbo la Fuoni  kugombea kwa pamoja na atakayeshinda ataongoza jimbo lakini wanatakiwa wajipange kupambana na wanaume,” anasema.

Mwanajuma Kassim Makame, viti maalum mkoa wa Kaskazini Unguja, anasema ugumu uliopo wa kugombea jimboni ni kupambana na wanaume lakini kwenye viti maalum unapambana na wanawake pekee.

Anasema pia changamoto nyingine ni gharama za kifedha kwa ajili ya kampeni ambapo jimboni ni gharama kubwa zaidi kuliko kwenye nafasi za viti maalum.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu Zanzibar (ZU), Dk. Sikujua Omar, anasema kwa vipindi hivyo wanawake watakuwa wamepata ujasiri na uzoefu na fedha za kuwawezesha kusimama majimboni kugombea nafasi za uongozi na kushinda.

Anasema viti maalum humwandaa mwanamke kwenda kwenye siasa za ushindani na ushawishi kwa wananchi kutokana na kujifunza kutoka kwa wengine.

Dk. Mzuri Issa Mkurugenzi wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake  (TAMWA) Zanzibar, anasema ushiriki wa wanawake katika uongozi ni hatua muhimu kuelekea usawa wa kijinsia katika uongozi na maendeleo ya kijamii.

Hata hivyo, anasema uwakilishi wa wanawake katika nafasi za uongozi ni mdogo, akitaja ukosefu wa  fedha ni moja wapo ya changamoto kubwa inayokwamisha wanawake kufikia malengo ya kuwa kiongozi.