Biashara mtandaoni zidhibitiwe, ni chanzo serikali kukosa mapato

Nipashe
Published at 09:01 AM Oct 23 2024
Biashara mtandaoni zidhibitiwe, ni chanzo serikali kukosa mapato
Picha:Mtandao
Biashara mtandaoni zidhibitiwe, ni chanzo serikali kukosa mapato

HIVI karibuni kumeibuka wimbi la biashara na mikopo kwa njia ya mtandao. Kupitia mikopo na biashara hizo, baadhi ya kampuni hizo zinatumia mitandao ya ya kijamii na simu za mkononi kuhamasisha watu kununua bidhaa na kukopa fedha.

Katika uhamasishaji huo, kampuni zinazouza vifaa, vingi vikiwa vya nyumbani kama vile sufuria, vyombo vya umeme na kudai kuwa malipo ni baada ya bidhaa kumfikia mteja.  Mteja anapouliza ofisi za kampuni hapewi majibu sahihi kwa kuwa hata anayefikisha mali ni wakala tu na si mmiliki wa duka au mfanyabiashara mwenye leseni ya kufanya hivyo. 

Kwa kampuni zinazokopesha fedha, zimekuwa na vivutio vingi kama vile riba ndogo na inalipwa kwa miezi sita au zaidi. Kampuni moja kwa mfano, ijajinasibu kwamba inakopesha Sh. 600,000 hadi 900,000 na mteja atalipa kiwango kidogo cha fedha kwa siku hadi kwa mwezi. Kwa mujibu wa kampuni hiyo, mtu akikopa 
 Sh. 500,000 kwa mfano, atarejesha Sh. 50 kwa siku au 1,400 kwa mwezi. 

Mikopo inayotolewa na kampuni hizo ambayo inatangazwa kwenye mitandao ya kijamii inatumika kama ulimbo kuwanasa baadhi ya Watanzania ambao wanachoangalia ni fedha na si kingine. Matokeo yake wanakuja kuyaona madhara baada ya kuwa wameshakopeshwa na kutambua kuwa ni kausha damu au mikopo umiza. 

Aidha, kwa kampuni za uuzaji na usambazaji wa vyombo vya majumbani, nazo zimekuwa zikitumia mwanya huo kuwaumiza wateja kwa kuwa baadhi ya vifaa huwa vya kiwango duni na huharibika muda mfupi huku wakitoa waranti ya mwaka mmoja. Chombo kinapopata matatizo, hawashughuliki na mteja na wanamwambia kanuni yao ni kwamba chombo kikishauzwa hakirejeshwi. Licha ya kutoa kauli hizo, kampuni hizo ambazo pia baadhi zimekuwa zikipitisha vyombo majumbani, zimekuwa hazitoi risiti kuonyesha kuwa ni walipakodi halali. 

Kutokana na kuwapo kwa biashara hizo na ukopeshaji wa kupitia mitandaoni, imebainika kwamba huo ni mwanya wa kuikosesha serikali mapato yatokanayo na kodi zinazotozwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA). Kwa kampuni zinazokopesha, zimebainika kuwa licha ya kutokulipa kodi halali, zinawatoza wananchi riba kubwa ambazo ni maumivu kwao. 

Mmoja wa waathirika katika ripoti ya uchunguzi kuhusu mikopo hiyo iliyochapishwa jana na juzi kwenye gazeti hili, anasema alikopa Sh. 50,000 lakini alilipa Sh. 250,000. Hata alipogoma kulipa baada ya kubaini kuwa ni riba kubwa kuliko alivyoambiwa wakati akishawishiwa kukopa, alidhalilishwa kwa kuwekwa picha yake kwenye mtandao wa kijamii.      

Katika kuonyesha mikopo hiyo kuwa imekithiri na inatweza na kudhalilisha utu wa mtu, Mbunge wa Viti Maalumu (Biashara mtandaoni zidhibitiwe, ni chanzo serikali kukosa mapato , Felista Njau, anasema katika utafiti wake alioufanya tangu mwaka 2020, amekutana na kero mbalimbali ikiwamo wakopeshaji kubadili majina ya taasisi hali inayoonesha kuna jambo lililojificha nyuma ya pazia. 

Anasema katika utafiti huo, amebaini kuwa mtu anakopa Sh. 50,000 lakini analipa mpaka Sh. 175,000 na wanaokopa, asilimia 65 ni wanawake ambao  wanaambiwa ni mikopo ya muda mfupi kuipata na haina usumbufu lakini baada ya kupata wanaanza kudaiwa na wale walio kwenye simu yake wanaarifiwa kuhusu jambo hilo. 

Jambo hili la mikopo umiza au kausha damu si migeni miongoni mwa Watanzana kwa sababu hata viongozi wakuu wa serikali wamekuwa wakilizungumza mara kwa mara huku wakiahidi kutunga sheria ya kuwabana wakopeshaji wa namna hiyo. 

Ni vyema sasa hatua zikachukuliwa na kukomesha mikopo hiyo ambayo inatweza utu wa mtu. Kwa  kuwa wakopeshaji hao wanafahamika, sheria kali zichukuliwe dhidi yao. Maneno sasa yanatosha, vitendo zaidi vinatakiwa.