Elimu madhara ya dawa za kulevya ianzie mashuleni

Nipashe
Published at 10:19 AM Aug 16 2024
Dawa za kulevya.
Picha: Mtandao
Dawa za kulevya.

MATUMIZI ya dawa za kulevya hasa kwa vijana yameathiri nguvu kazi na kusababisha wengi wao kuishia mitaani na kufanya vitendo vya uporaji ili wapate pesa ya kununulia dawa hizo.

Wazazi wamekuwa katika wakati mgumu hasa baada ya kujitoa kuwasomesha vijana wao na kinyume walivyotarajia kuwa watakuwa msaada, wanageuka kuwa mzigo kwa familia.

Wengi wa vijana hao wanaharibika kutokana na makundi wanayoambatana nayo na kupata vishawishi vya kutumia dawa hizo.

Baadhi ya wazazi wanatumia gharama kubwa kuwasomesha watoto wao nje ya nchi, lakini wakirudi nchini tayari wameshaathirika na madawa ya kulevya. 

Kutokana na tatizo hilo, serikali imeamua kuchukua hatua ili kudhibiti kikamilifu matumizi ya dawa za kulevya nchini, kwa kupanga kuhamishia elimu inayoendelea kutolewa katika maeneo mbalimbali ikiwamo kuipeleka kwenye shule za msingi, sekondari na vyuo vikuu kama ilivyo kwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU).

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwa jijini Mwanza katika kilele cha maadhimisho ya kitaifa ya kupiga vita dawa za kulevya duniani alisema “ni lazima tuimarishe mikakati yetu ya kukabiliana na mapambano haya na Serikali imejikita katika kutoa elimu ili jamii ifahamu, na tutakwenda kuanzisha klabu katika shule za msingi, sekondari mpaka vyuo vikuu kama walivyofanya TAKUKURU ili kupunguza kama si kumaliza kabisa tatizo hili."

Pia, vijana wa Kitanzania wametakiwa kuachana na matumizi na biashara ya dawa za kulevya na badala yake waungane katika kufanya shughuli halali za kiuchumi ili wajiletee maendeleo katika ngazi ya familia, jamii na hata taifa.

Kadhalika, jamii inatakiwa kuelimishwa zaidi kuhusu athari za matumizi ya dawa hizo na kuwa njia hiyo itakuwa mwarobaini wa tatizo hilo sugu pamoja na kuwawezesha waliotoka kwenye uraibu (waraibu) ili waweze kujumuika na wenzao na wafanye kazi itakayowawezesha kujisimamia.

Kuhusu taarifa iliyotolewa na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda ya hali ya dawa za kulevya katika Mkoa wa Mwanza kuanzia mwaka 2018 hadi 2023, wananchi waliopatikana na bangi ni 1797, mirungi 294, cocaine, heroine na nyingine ni 51 na kufanya jumla ya dawa zote kuwa 2142.

Takwimu hizi zinabainisha kwamba biashara na matumizi ya dawa za kulevya mkoani Mwanza ni kubwa na inahitaji msukumo mkubwa kutoka kwa serikali pamoja na wadau mbalimbali ili kuendelea kupambana na wazalishaji, wasambaji na watumiaji wa dawa hizo.

Ukiangalia vijana wengi wanao athirika ni kutoka katika majiji ambako hufanyika mambo mengi ya starehe na hupata vishawishi vya kujiingiza kwenye matumizi hayo kama sehemu ya starehe.

Aidha, vijana wanao athirika ni wa jinsi zote na kusababisha wazazi wengine kupata msongo wa mawazo kutokana na hali wanayopitia kwani wengine hugeuka wezi kwenye nyumba zao ili wapate pesa za kuwawezesha kununua dawa hizo.

Vita ya kupambana na dawa za kulevya ni kubwa kwa sababu inahusisha wafanyabiashara wakubwa wenye uwezo kipesa ambao wanaweza kutumia nguvu yao ya pesa kuendeleza biashara hiyo.

Jambo la muhimu kabisa ni elimu kwa vijana hasa katika shule ambako wengi hushawishiwa kutokana na uelewa wao mdogo wa kufahamu lipi zuri na lipi baya.