Mauaji yanakichafua kisiwa hiki cha amani

By Moshi Lusonzo , Nipashe
Published at 10:45 AM Sep 11 2024
Bendera ya Tanzania.
Picha:Mtandao
Bendera ya Tanzania.

TANGU mjumbe wa Sekretarieti wa CHADEMA Taifa, Ali Kibao, kuuawa kikatili wiki iliyopita Septemba 6, hali ya wasiwasi inazidi kutanda , watu wengi wakipata hofu ya usalama wao hasa wanaharakati na watetezi wa demokrasia.

Kifo hicho cha kushtua kimezidi kuleta utata kuhusu matukio mengi ya utekaji, kuua na kutoweka kwa baadhi ya watu ambao hadi sasa hakuna taarifa kamili kuhusu wapi walipo na kitu gani kimewakabili.

Kitendo cha kutekwa Kibao akiwa ndani ya basi akielekea  Tanga tena kwa mtutu wa bunduki na hatimaye mwili wake kukutwa umetupwa eneo la Ununio mkoani Dar es Salaam,  ni kuongeza taharuki, hofu, wasiwasi na kuipa Tanzania jina jingine linaloweza kutofautiana na kisiwa cha amani.

Watu wanaweza kuamini kuwa wanaofanya unyama huo wana uhuru mkubwa wa kutenda chochote na lolote , wakati wowote na mahali kokote bila hofu.

Watanzania wengi wana maswali mengi ambayo hayana majibu, wamebaki na tumaini moja pekee nalo ni kutekelezwa maagizo ya  Rais Samia Sulu Hassan, ambaye ameamuru kufanyika uchunguzi wa haraka na kina kuhusu tukio hilo.

Ni wazi Rais Samia, amezungumza kutoka moyoni na anahisi maumivu makali kutokana na matukio ya aina hayo kuendelea nchini yanayofanywa na watu waliojipachika jina la wasiojulikana.

Baada ya kauli yake hiyo ambayo aliagiza vyombo vya uchunguzi kumpelekea  taarifa ya kina kuhusu tukio hilo, ni wazi majibu yatapatikana na kuwapa auheni wengi wanakata tamaa na kuzidiwa na hofu.

Ukweli mama ameshazungumza na hakuna ambaye anaweza kwenda kinyume na hitaji lake, na ndivyo wengi wanatamani kuona ili kukata kiu yao ya muda mrefu ambayo inazidi kuwatesa wanaharakati na wanasiasa.

Kama ilivyo kwa Rais Samia ambaye naye anatamani kujua nini kipo ndani ya tukio hilo, Watanzania pia wanataka kujibiwa maswali ambayo yanawapa shida kupata majibu ikiwamo watu gani wametekeleza unyama huo? Ni nani yuko nyuma na wanaofanya matukio hayo? Sababu yake ni nini?.

Pia, wanataka kufahamu kama watu hao wasiojulikana wanaweza kutekeleza misheni yao kwa uhuru hata katika maeneo ya umma, ndani ya chombo cha usafiri  kilichosheheni abiria.

Kuna wanaonyooshea kidole vyombo vya dola kuwa pengine vinahusika, lakini majibu atakayopelekewa Rais Samia yanaweza kutoa mwanga na kisha kuwaondoa shaka raia ambao kwa sasa wamebaki njia panda.

Ukweli ni kwamba uchunguzi huo ambao umeagizwa kufanywa na vyombo vya dola, utarudusha hali ya kuaminiana ambao kwa sasa umeonekana kutoweka baada ya kushamiri kwa matukio ya  watu kutekwa na kuawa kimya kimya.

Kimsingi Watanzania wanamuunga mkono kwa dhati Rais Samia kutaka kupata maelezo ya kina na kuhusu kilichotokea kabla na baada ya kuawa Kibao ambaye familia yake na taifa kwa ujumla bado lilihitaji mchango wake.

Pamoja na wengi kutokubaliana na hali inavyoendelea, lazima tujiweke kando na vitendo vyovyote vya kuingilia mwenendo wa uchunguzi na ikiwezekana wale wenye vielelezo au taarifa zinakazowabaini wahusika kujitokeza kwenda kuwasilisha sehemu husika.

Hakuna njia nyingine nzuri ya kurahisisha mchakato huo, bali ni kushirikiana na timu inayochunguza tukio hilo na kisha majibu yake kuwasilishwa kwa rais.

Ni wazi Rais hajatoa agizo hilo kwa kujifurahisha, bali anaona umefikiwa wakati matukio ya aina hayo kukomeshwa kwa ajili ya maslahi ya nchi na uimara wa demokrasia na amani ya taifa. 

Hakuna Mtanzania anayekubali kuona vitendo vya aina hii vikiendelea kuiumiza nchi, hivyo ni lazima vyombo vya dola vinavyohusika kulinda usalama wa watu kuingilia kati ili watu waendelee kuishi kwa amani na kufanya shughuli zao kwa uhuru.

Wakati umefika kwa jeshi la polisi ambalo wengi wanalilalamikia kwa kutofanya kazi ipasavyo katika kukabiliana na vitendo vya utekaji, kubadili mbinu zake kwa kuwatufuta watu hao na kuwakamata na kuwafikisha katika vyombo vya sharia kabla hajatekeleza malengo yao.

Waanzishe madawati huru ambayo wananchi wanaweza kwenda kutoa taarifa bila kuwa na hofu au kuonesha viashiria ambavyo vitabaini kufuatiliwa, kuwaona  watu wanaotiliwa shaka.