Matukio ya utekaji, mauaji yanafikirisha

Nipashe
Published at 11:10 AM Sep 10 2024
Matukio ya utekaji.
Picha: Mtandao
Matukio ya utekaji.

KURIPOTIWA kwa matukio ya utekaji na mauaji ya kila mara katika maeneo mbalimbali nchini yanaleta hali ya wasiwasi na amani iliyozoeleka imeanza kuingia doa.

Tanzania inasifika duniani kuwa ni nchi ya amani na ndio sababu wageni wengi wanamiminika kuja kuitembelea.

Matukio haya yaliyoanza kujitokeza yanaleta hali ya wasiwasi na kusababisha wananchi kukosa amani wanapofanya shughuli zao kwa kuwa hawajui ni wakati gani wanaweza kupatwa na mkasa.

Tanzania haikuzoea kusikia kila kukicha matukio ya kutisha na ya kusikitisha yakiwamo ya utekaji, ubakaji na mauaji.

Kuibuka kwa matukio haya kumesababisha kila mtu kumnyooshea kidole mwenzake bila kujua kiini cha tatizo hilo ni nini.

Takribani miaka mitatu iliyopita kuliibuka matukio ya watu kutoweka wakiwamo waandishi wa habari na wengine mpaka leo hawajulikani walipo.

Hali ilirudi kuwa shwari, lakini sasa yameanza kuibuka tena na kwenye jamii yamepamba moto kutokana na taarifa zinazoripotiwa kila mara matukio hayo kufanyika.

Kinachosikitisha zaidi hata watoto wasiokuwa na hatia wameingizwa kwenye matukio hayo na kupotezewa maisha yao.

Taarifa za hivi karibuni zinaeleza mtoto na mama yake walivyofanyiwa vitendo vya ukatili na kisha kuuawa.

Kwa hivi karibuni Mkoa wa Dodoma, kumeripotiwa matukio kadhaa ya kinyama na mauaji na watu kuhoji kuna upepo gani mbaya umeikumba nchi yetu.

Wanaotekeleza unyama huo haifahamiki kama wanafanya kwa kulipiza kisasi au kwa sababu za kishirikina.

Wakati uchunguzi ukiendelea kwa matukio yaliyofanyika katika mkoa huo, mengine yanajitokeza ya utekaji wa kada wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), ambaye ilidaiwa alichukuliwa na watu wasiojulikana wakati akiwa kwenye basi la abiria.

Huku Jeshi la Polisi likifanya uchunguzi kuhusu tukio hilo, habari zinaeleza kuwa kada huyo amekutwa ameuawa eneo la Ununio, jijini Dar es Salaam.

Hakika tukio hili limezua taharuki kubwa kwa kuwa inaelezwa kuwa, waliomchukua walikuwa wamebeba silaha za moto na walimfunga pingu kabla ya kumshusha kwenye basi hilo alilokuwa akisafiri nalo.

Watu kutekwa, kutoweka na kuondolewa uhai sasa zimekuwa taarifa zinazotawala vyombo vya habari pamoja na mitandao ya kijamii.

Matukio haya yalianza taratibu, lakini yanakoendelea yanaweza kuwa makubwa na kusababisha wananchi kuhofia kutembea kwa amani kwenye nchi yao.

Jeshi la Polisi linafanya uchunguzi kuhusu matukio hayo na imani ya wananchi kuwa waliofanya vitendo hivyo vya kinyama watakamatwa ili sheria ichukue mkondo wake.

Damu za watu haziwezi kupotea bure, hata kama waliofanya vitendo hivyo watakuwa wamekimbia kwenda maeneo ya mbali, lazima watajulikana.

Wananchi pia ni lazima tutoe ushirikiano kulisaidia Jeshi la Polisi kuwapata wahalifu hao ili nchi yetu isiingie doa.

Sisi sote ni walinzi na tunapotoa ushirikiano kazi ya kupatikana kwa wahalifu hao itakuwa rahisi. Hakuna anayependa kuona uhai wa mtu ukiondolewa kwa sababu za chuki na ubinafsi au ushirikina.

Tanzania ni nchi ya kisiwa cha amani na amani hii iendelee kudumishwa ili tuendelee kupokea wageni wanaokuja kujifunza kwetu jinsi ya kuishi kwa umoja na upendo.

Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Afrika.