KATIKA toleo letu la jana, tulikuwa na ripoti maalumu kuhusiana na kadhia ya udhalilishaji mtandaoni wagombea wa nafasi za kisiasa nchini, waathirika wakuu wakiwa ni wanawake.
Baadhi ya wanawake waliokumbwa na udhalilishaji huo, wamesema haufanyiki pasi na kujua madhara yake, bali ni mikakati ya makusudi ya baadhi ya watu kudhoofisha ushiriki wao kwa kuwatia woga na kuwakatisha tamaa kujihusisha na siasa.
Wanasiasa hao wametaja madhila wanayopitia katika mitandao ya jamii, hasa wakati wa mchakato wa uchaguzi, yanajumuisha lugha za matusi, wenza wao kutumiwa ujumbe kwamba wake zao wana uhusiano wa kimapenzi na viongozi wa kisiasa na wale wasiokuwa na watoto, kudhalilishwa kwa "kushindwa kuwazalia waume zao".
Ni madhila waliyoyataja yanawafanya wanawake waogope na kuona kuwa siasa zitaacha doa kwao, hivyo kuwa kikwazo kikubwa kufikia uwakilishi wa 50/50 katika vyombo vya uamuzi na kufikia usawa wa kijinsia nchini.
Wameitaja mitandao ya kijamii kuwa "sumu kwa wanawake kisiasa", wakisisitiza udhalilishaji huo ni miongoni mwa mambo yanayorudisha nyuma mikakati ya kitaifa inayolenga kufikia usawa wa kijinsia katika siasa, takwimu rasmi za kiserikali zikionesha kundi hilo halina uwakilishi mkubwa katika vyombo vya uamuzi.
Mathalani, ripoti ya iliyokuwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ya mwaka 2020, inaonesha wanawake waliochaguliwa kwa nafasi za udiwani walikuwa asilimia 6.58 (260 kati ya madiwani 3,953), viti maalumu walikuwa 1,374 katika halmashauri 184 sawa na asilimia 24.59. Kwa jumla, wanawake walikuwa asilimia 29.24 ya madiwani wote nchi nzima.
Ripoti ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa Mwaka 2019 pia inaonesha kuwa kati ya nafasi 11,915 za wenyeviti wa vijiji, wanawake walishinda nafasi 246 sawa na asilimia 2.1, huku wanaume wakishika asilimia 97.9 ya nafasi hizo. Kati ya nafasi 4,171 za wenyeviti wa mitaa, wanawake walishinda nafasi 528 sawa na asilimia 12.6.
Vilevile, Taasisi ya Kitaifa ya Kidemokrasia (NDI) inaonesha kuwa katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020, wanawake waliochaguliwa kwa nafasi za ubunge ni asilimia 9.5, wabunge wa viti maalumu ni asilimia 29, hivyo kufanya jumla ya wabunge wanawake kuwa 142 kati ya 393.
Nipashe pia tunatambua kuna utafiti wa mwaka 2021 uliofanywa na Umoja wa Mabunge ya Afrika (APU), ukihusisha wabunge wanawake 224 kutoka nchi 50, ikiwamo Tanzania. Ulibaini asilimia 80 ya waliohojiwa walipitia ukatili wa kisaikolojia, huku asilimia 46 wakikumbana na ukatili wa kijinsia mtandaoni.
Tunatambua pia kwamba, ripoti ya Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) ya mwaka 2023, inaonesha kuwapo ongezeko kubwa la udhalilishaji kidijitali na ukatili wa kijinsia mtandaoni nchini, wanawake wakiwa walengwa wakuu, kwa asilimia 56.
LHRC ina lingine la ziada; licha ya unyanyasaji huo, wanawake hawatafuti msaada wa kisheria. Takwimu rasmi za kituo hicho zinaonesha asilimia 65 ya wateja waliotembelea kituo kusaka msaada wa kisheria mwaka huo, walikuwa wanaume.
Kudhalilisha wagombea wanawake mtandaoni si tu kunawanyima nafasi ya kushiriki uchaguzi, bali pia kunawaathiri kisaikolojia na hata kijamii, hivyo mamlaka husika zichukue hatua kudhibiti kadhia hii ikizingatiwa hivi sasa nchi iko katika mchakato wa uchaguzi.
Wadhalilishaji wachukuliwe hatua kwa mujibu wa hatua zilizowekwa kisheria ikiwamo Sheria ya Kanuni za Adhabu, Sura 16, inayoelekeza adhabu ya faini, au/na kifungo cha hadi miaka miwili gerezani kwa jinai hiyo.
Vilevile, udhalilishaji unaofanywa dhidi ya wagombea wanawake nchini, unakinzana na Sera ya Maendeleo ya Wanawake na Jinsia Tanzania ya Mwaka 2000 inayolenga kuweka mazingira wezeshi, kutatua vikwazo dhidi ya wanawake na kuleta haki na usawa ili kundi hilo lishiriki kikamilifu na kwa ufanisi katika programu na miradi ya maendeleo.
Kitendo hicho pia kinakwaza utekelezaji wa Lengo Na. 5 la Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDG) linalozitaka nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa (UN) kuhakikisha zinatilia mkazo usawa wa kijinsia.
Tanzania pia imeshatia saini na kuridhia Mkataba wa Kimataifa wa Kuondoa Aina zote za Ubaguzi dhidi ya Wanawake (CEDAW) wa Mwaka 1979, unaoelekeza kuondoa aina zote za ubaguzi na uonevu kwa wanawake.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED