Ulaji sahihi unavyopunguza hatari ya magonjwa yasiyoambukiza

Nipashe
Published at 10:46 AM Aug 15 2024
 Shirika la Afya Duniani (WHO).
Picha: WHO
Shirika la Afya Duniani (WHO).

MAGONJWA yasiyoambukiza yanaelezwa kusumbua watu wengi hasa wenye umri mkubwa kutokana na kutozingatia vizuri mtindo wa maisha yao.

Magonjwa yasiyoambukiza ni yale ambayo hayasambazwi kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mwingine kwa kuwa hayana vimelea vinavyohusiana na magonjwa hayo.

Katika nchi zinazoendelea, Tanzania ikiwa mojawapo ajali za barabarani na madhara yatokanayo na vilevi yamewekwa kwenye orodha ya magonjwa yasiyoambukizwa.

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), magonjwa yasiyoambukiza ndio yanayoongoza kwa kusababisha vifo duniani.

Utafiti unasema asilimia 72.8 duniani ya vifo vinasababishwa na magonjwa yasiyoambukiza na shinikizo la damu limekuwa kichocheo kikubwa.

Utafiti huo uliofanywa na Nature mwaka 2007 umeripoti kuwa magonjwa yasiyoambukiza yanaua kwa kasi zaidi kulinganisha na yale yanayoambukiza.

Kutokana na takwimu hizo za kidunia kwa hapa nchini katika utafiti uliofanywa mwaka 2012, unaonesha kuwa asilimia 92.6 ya Watanzania ambao vipimo vyao vya shinikizo la damu vina walakini, hawajaanza kutumia dawa, hali inayowafanya kuwa katika hatari ya kupata magonjwa mengine yasiyoambukiza.

Ulaji chakula bila kuzingatia kanuni za afya umeelezwa kuwa chanzo kinachochangia magonjwa hayo kuwakumba watu wengi.

Hivi sasa hospitali nyingi zinapokea wagonjwa wenye magonjwa yanayotokana na tatizo la shinikizo la damu, moyo, figo na mengine ambayo chanzo chake ni mtindo wa maisha wanayoishi.

Wataalamu wa afya mara kwa mara wanashauri watu kuzingatia ulaji uliosahihi na kufanya mazoezi ili kujikinga na maradhi hayo.

Kwa mujibu wa wataalamu hao magonjwa yasiyoambukiza yanatumia gharama kubwa katika matibabu ya wagonjwa kulinganisha na magonjwa mengine.

Magonjwa hayo yanaweza kudhibitiwa kwa watu kufuata kanuni za afya ikiwamo pia kucheki afya zao mara kwa mara ili kujua mwenendo wao.

Kuna wakati mtu anakwenda hospitali kutibiwa tatizo lingine, lakini anapofika na kuangaliwa mwili wake anakutwa na tatizo kubwa.

Utafiti unaeleza kuwa umri wa kuishi kwa wanawake ni miaka 69 na wanaume umepungua kwa sasa wanaishi miaka 62 kwa ajili ya changamoto mbalimbali ikiwamo mabadiliko ya tabianchi, mazingira na mabadiliko katika maendeleo.

Magonjwa yasiyoambukiza imeelezwa kuwa ni changamoto hasa katika umri wa wazee na kila mara kumekuwa kukitolewa elimu kwa kuwashirikisha watu wenye umri huo kuwakumbusha kufanya mazoezi ya viungo ambayo yanasaidia kutoa sumu mwilini na kuimarisha mifupa na nyonga.

Moja ya mambo yanayochangia kuongezeka kwa magonjwa hayo ni mabadiliko ya taratibu za kimaisha zinazohusisha matendo yanayoweza kusababisha magonjwa.

Moja wapo ni kukaa muda mrefu sehemu moja kama vile ofisini au darasani na kutojihusisha katika shughuli za michezo.

Ulaji usiofaa. Kula chakula kuzidi mahitaji ya mwili, kula chumvi na sukari kuliko mahitaji ya mwili ni vitu vinavyochangia kuongezeka kwa magonjwa hayo.

Dalili za magonjwa yasiyoambukiza ni watu kujiona kuchoka bila sababu, kichwa kuuma mara kwa mara, macho kutoona vizuri, kushikwa na kizunguzungu mara kwa mara, kutokwa na damu kwenye fizi mara kwa mara, miguu na mikono kuwa na maumivu kama ya kuwaka moto na nyingi zinazofanana na hizo.

Mtu akishaona dalili hizo ni bora akimbilie hospitali na kubadili mtindo wake wa maisha.