Fadlu: Hatutaidharau Pamba Jiji

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 09:44 AM Nov 20 2024
Kocha Mkuu wa Simba, Fadlu Davids.
Picha:Mtandao
Kocha Mkuu wa Simba, Fadlu Davids.

KOCHA Mkuu wa Simba, Fadlu Davids, amesema hawatoidharau Pamba Jiji kwa sababu tu haifanyi vema kwenye mechi zake za Ligi Kuu, badala yake wamejindaa vizuri na kuweka nguvu kubwa katika mchezo huo utakaochezwa, Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza, Ijumaa ijayo.

Akizungumza juzi jijini Dar es Salaam, kocha huyo raia wa Afrika Kusini, alisema waliiomba mechi hiyo kwa makusudi kwa ajili ya kuwapa mazoezi, utimamu wa mwili na uchangamfu wachezaji wake kabla ya kuivaa Bravo do Maquis ya Angola katika mchezo wa raundi ya kwanza, Kombe la Shirikisho Afrika hatua ya makundi utakaopigwa, Uwanja wa Benjamin Mkapa, Novemba 27, mwaka huu.

Alisema kwa sababu waliuomba, basi wataufanyia kazi kwa jinsi walivyouhitaji, yaani uwe wa maandalizi na pia kuhitaji pointi tatu za kuzidi kukaa juu kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

"Ni mchezo muhimu sana kwetu, tuliuhitaji na tunautaka tuucheze kwa nguvu kama vile tunacheza mechi ya kimataifa, kwa sababu tunajiandaa na hilo, kwa kutambua hilo, nilitaka mechi ya kirafiki kwa ajili ya mechi ya Pamba Jiji," alisema Fadlu.

Simba ilicheza mechi yake ya kirafiki mwishoni mwa wiki dhidi ya KMC kwenye Uwanja wa KMC Complex, Mwenge, Dar es Salaam, ambapo kwa mujibu wa Fadlu ulikuwa ni wa kujiandaa dhidi ya Pamba Jiji, huku wa Pamba ni wa kujiandaa dhidi ya Bravo do Maquis.

Awali mchezo huo uliahirishwa na Bodi ya Ligi, lakini uongozi wa Simba uliomba urudishwe ambapo taarifa zinasema Fadlu mwenyewe ndiye aliyeomba.

Kocha huyo pia alitoa siri ya kuichagua KMC na si timu nyingine, akisema anavutiwa na aina yao ya soka ambayo aliona inamfaa kwa ajili ya kuwatengeneza vijana wake.

"Katika timu zote alizoziona Tanzania, wao ndiyo wanacheza soka safi ambalo kama ukicheza nao kuna kitu unakipata kwenye masuala ya ufundi na ilikuwa hivyo, tulipata kipimo sahihi kweli," alisema.

Kikosi cha Simba kinatarajiwa kuondoka Alhamisi kwenda Mwanza kwa ajili ya mchezo huo, ikiwa kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu kwa pointi 25, ikicheza michezo 10.

Pamba Jiji ambayo itakuwa nyumbani ipo nafasi ya 15 ya msimamo wa Ligi Kuu, ikiwa na pointi nane kwa michezo 11, baada ya kushinda mchezo mmoja tu mpaka sasa, sare tano na kupoteza mitano, lakini pia ikiwa haijashinda mchezo wowote ikicheza uwanja wake wa nyumbani, CCM Kirumba.