BAADA ya kumaliza dabi yao Jumamosi iliyopita, Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, vigogo wa soka nchini, Simba na Yanga leo watashuka tena dimbani kucheza mechi zao za Ligi Kuu Tanzania Bara.
Hata hivyo, wakati Kocha Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi akisema haoni kama timu yake inaweza kushinda idadi kubwa ya mabao leo itakapocheza dhidi ya JKT Tanzania saa 1:00 usiku, Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam, wa Simba Fadlu Davids, amesema wamekwenda Mbeya kusaka pointi tatu ili kukaa kwenye reli ya kusaka ubingwa, ambapo watashuka, Uwanja wa Sokoine, saa 10:00 jioni kucheza dhidi ya Prisons, akiwatahadharisha waamuzi kuchezesha kwa haki, akitaka pia VAR itumike kwenye michezo ya ligi.
"Nafikiri hatuwezi kushinda mabao mengi katika mchezo huu, ikumbukwe hawa msimu uliopita tulitoka nao sare.
"Nimeiangalia timu hii, ina uwiano mzuri wa kushinda ikicheza nyumbani, imepoteza mchezo mmoja tu, ikionekana ni ngumu kufungika na mabeki wake wako vizuri, hivyo tumelifanyia kazi, tunahitaji kupambana ili kushinda tena mchezo, nafikiri itakuwa mechi ngumu inabidi tuwe makini, hawa jamaa mashambulizi yao wanaanzia nyuma na wanapenda kushambulia pembeni na pasi ndefu pia," alisema Gamondi.
JKT Tanzania inashika nafasi ya sita kwenye msimamo wa ligi, ikicheza michezo saba, ikishinda miwili, sare nne, ikipoteza mchezo mmoja.
Yanga ambayo itaingia uwanjani ikiwa na kumbukumbu ya kuwachapa watani zao wa jadi bao 1-0 Jumamosi iliyopita, itacheza mchezo wake wa sita wa ligi, ikiwa nafasi ya pili, imeshinda mechi zote tano, ikiwa ni timu pekee ambayo wavu wake haujaguswa mpaka sasa.
Kocha Mkuu wa JKT Tanzania, Ahmad Ally, amekiri kuwa anakwenda kucheza mchezo mgumu dhidi ya Yanga.
"Ni timu bora kwa sasa hapa nchini, na inaleta ugumu hata kwa baadhi ya timu nje ya nchi, ukiangalia hata mchezo uliopita dhidi ya Simba, aliwatoa kina Pacome Zouzoua, Prince Dube, na Stephane Aziz Ki, lakini aliingiza wachezaji ambao walikwenda kubadili mchezo, hivyo kazi yetu kubwa itakuwa kwenye kuuzuia na kupambana na ubora wao, kwa bahati nzuri ninao aina ya wachezaji hao," alisema kocha huyo.
Fadlu, Kocha Mkuu wa Simba amesema timu yake imejipanga vema, licha ya kucheza mechi ngumu dhidi ya Yanga kwenye uwanja uliokuwa unateleza kutokana na mvua, lakini haijalishi badala yake wamekwenda kuchukua pointi tatu, huku akiiomba mamlaka ya soka nchini kuwa na VAR kwenye Ligi Kuu kwani wamekuwa waathirika wa makosa ya waamuzi.
"Tulicheza mchezo mgumu dhidi ya Yanga, tumepumzika siku mbili tu pamoja na kusafiri, tuna kazi ya kufanya, tunaiheshimu Prisons lakini tumekuja Mbeya kuchukua pointi tatu, hili litawezekana kama maamuzi yatafanyika sahihi.
"Tulinyimwa penalti mbili na mchezaji mmoja wa Yanga alipaswa kupewa kadi nyekundu kwenye mchezo uliopita, Ligi ya Tanzania kubwa kama hii sasa inahitaji VAR, itafanya mpira wa nchini kukua kwani kutakuwa na maamuzi sahihi na kila mmoja atapata anachostahili, kama si mechi zote hata kwenye michezo mikubwa, nchi nyingi za Afrika sasa zinatumia na imeleta athari chanya," alisema kocha huyo.
Nahodha wa timu hiyo, Mohamed Hussein "Tshabalala', amesema wanatambua kuwa huwa wanapata tabu sana wanapocheza dhidi ya Prisons kwenye uwanja huo, lakini safari hii watahakikisha hawaruhusu bao.
Msimu uliopita, Simba ililala mabao 2-1 katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwenye uwanja huo.
"Tumekuwa na matokeo magumu sana tukiwa hapa Mbeya, hilo tunalijua na tumekuja kupambana na jukumu la kwanza ni kuhakikisha haturuhusu bao," alisema.
Mbwana Makata, Kocha Mkuu wa Prisons, alikubali muziki wa Simba, akisema waliiona ikicheza dhidi ya Yanga, hivyo wataingia kwa tahadhari.
"Maandalizi ni mzuri, tunawaheshimu ni moja ya timu nzuri na hata mchezo dhidi ya Yanga walicheza vizuri mno, walikuwa wanacheza na kubadilika, wana wachezaji wenye uzoefu kwa hilo tunawaheshimu, kwa maana hiyo tumetengeneza mpango mkakati mbele ya timu iliyokuwa bora," alisema.
Simba ina pointi 13, ikiwa kwenye nafasi ya nne ya msimamo wa Ligi Kuu, ikicheza michezo sita, Prisons ikishika nafasi ya 12, ikikusanya pointi saba kwa mechi saba ambazo imecheza mpaka sasa.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED