JKT Queens kileleni TWPL

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 12:22 PM Dec 19 2024
Kipa wa JKT Queens, Najiath Abbas (kushoto), akiwania mpira dhidi ya mshambuliaji wa Yanga Princess, Arieth Udong, katika mechi ya Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania iliyochezwa kwenye Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam juzi. JKT Queens ilishinda mabao 2-0.
Picha: Mpigapicha Wetu
Kipa wa JKT Queens, Najiath Abbas (kushoto), akiwania mpira dhidi ya mshambuliaji wa Yanga Princess, Arieth Udong, katika mechi ya Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania iliyochezwa kwenye Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam juzi. JKT Queens ilishinda mabao 2-0.

BAADA ya kupata ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Yanga Princess, straika wa JKT Queens, Fatuma Makusanya, amesema siri ya mafanikio ya kikosi chao ni kufuata vyema maelekezo ya benchi la ufundi.

JKT Queens sasa imefikisha pointi 17 ikifuatiwa na mabingwa watetezi, Simba Queens yenye pointi 16, lakini imecheza mechi moja pungufu.

Akizungumza na gazeti hili baada ya mechi hiyo iliyochezwa kwenye Uwanja wa KMC Complex juzi, Makusanya alisema utulivu na kufuata maelekezo wanayopewa mazoezini ndio yamewasaidia kupata ushindi.

"Kikubwa ni kufanya kile ambacho tunakifanya mazoezini, nilipoingia uwanjani nilikuwa nawaza kufanya kile nilichoelekezwa na kocha, na ndio kimesaidia kufunga bao," alisema Makusanya.

Aliongeza licha ya ushindi waliopata, bado amekiri ligi ya msimu huu ni ngumu na ina ushindani.

"Nitasema msimu ni mzuri pale ligi itakapomalizika, siwezi kusema kwa sasa kwa sababu bado hatujamaliza msimu, ila ligi ni ngumu na ina ushindani katika kila mechi," nyota huyo wa zamani wa Twiga Stars alisema.

Ligi hiyo itaendelea tena keshokutwa kwa Mashujaa Queens kuwakaribisha Simba Queens kwenye Uwanja wa Isamuhyo.