MBIO za kuwania taji la Ligi Kuu Tanzania Bara zinatarajia kuendelea tena kwa wenyeji Namungo FC kuwakaribisha JKT Tanzania katika mechi itakayochezwa leo kwenye Uwanja wa Majaliwa ulioko Ruangwa mkoani, Lindi.
Namungo watashuka katika mechi hiyo wakiwa na kumbukumbu ya kupata ushindi wa ugenini wa mabao 3-2 dhidi ya KenGold ya Mbeya Jumapili iliyopita.
Kuelekea mechi hiyo, Kocha Mkuu wa Namungo, Juma Mgunda, ameahidi timu yake itaendeleza wimbi la ushindi.
Mgunda amesema ushindi waliopata ugenini umewafanya vijana wake wawe na morali zaidi na hali ya kujiamini, hivyo anatarajia kupata ushindi mwingine leo watakaposhuka kwenye ardhi ya nyumbani.
"Ule ushindi tulioupata dhidi ya KenGold umetusaidia sana, umewafanya vijana wangu kupata morali na kuona kumbe wakipambana wanaweza kupata matokeo mazuri, kutokana kuruhusu mabao mawili hadi kurudisha yote na kufunga matatu si mchezo, lakini tulifanya hivyo.
Tunajua JKT Tanzania ni moja kati ya timu ngumu, hasa kwenye eneo lao la ulinzi, lakini sisi tumejipanga na watarajie mechi ngumu kutoka kwetu," alisema kocha huyo wa zamani wa Coastal Union na Simba.
Ofisa Habari wa JKT Tanzania, Masau Bwire, ametamba wako tayari kuwapa burudani ya kutosha mashabiki wa mkoa wa Lindi na vitongoji vyake, lakini pia akiwaonya Namungo wajiandae kupata fedheha mbele ya mashabiki wao.
"Tunawaomba mashabiki wa mkoa wa Lindi, waje Uwanja wa Majaliwa kuangalia soka safi linalotandazwa na JKT Tanzania, lakini nawaambia Namungo leo wataadhirika kwa kupata fedheha mbele ya mashabiki wao kwa sababu hatutawaacha salama, tumekuja kuchukua pointi tatu," alitamba Bwire.
Utakuwa ni mchezo wa 15 kwa Namungo, ikimaliza michezo yake ya mzunguko wa kwanza huku ikiwa nafasi ya 12 ya msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara kabla ya mechi ya leo, JKT Tanzania ambayo itacheza mechi yake ya 14, ikiwa nafasi ya saba baada ya kujikusanyia pointi 19 kibindoni.
Azam FC ambayo pia imemaliza mechi zake za mzunguko wa kwanza inaongoza msimamo wa ligi hiyo ikiwa na pointi 33 ikifuatiwa na Simba yenye pointi 31 huku Singida Black Stars yenye pointi 30 ikifuatia.
KenGold ya Mbeya yenye pointi sita na imecheza mechi 15 inaburuza mkia katika msimamo wa ligi hiyo inayoshirikisha timu 16 kutoka mikoa mbalimbali.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED