Ramovic aanza kwa mkwara mzito Yanga

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 09:30 AM Nov 20 2024
Ramovic aanza  kwa mkwara  mzito Yanga
Picha:Mtandao
Ramovic aanza kwa mkwara mzito Yanga

HATIMAYE Kocha Mkuu mpya wa Yanga, Sead Ramovic, raia wa Ujerumani ameanza kukinoa kikosi hicho kwa kishindo na mkwara mzito, kuelekea kwenye mchezo wa raundi ya kwanza, Ligi ya Mabingwa Afrika, hatua ya makundi dhidi ya Al Hilal Omrudman ya Sudan, utakaopigwa, Novemba 26, mwaka huu, kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Kwanza kabisa kocha huyo aliingia kwa mara ya kwanza juzi kwenye Uwanja wa Avic Town uliopo Kigamboni, Dar es Salaam na kuanza kuukagua kabla ya kufanya kitu chochote kile, akiwa ameongozana na kocha wake msaidizi mpya, Mustapha Kodro, raia wa Bosnia & Herzegovina.

Aliingia na kutembea akizunguka maeneo ya uwanja na kuna wakati alikuwa akiinama chini na mkono wake ulikuwa unakagua ubora wa nyasi na udongo ndani ya uwanja huo.

Baadaye alionekana kunong'ona kitu na msaidizi wake na baadaye walikwenda kuungana na benchi zima la ufundi, akiwamo meneja wa timu hiyo, Walter Harrison, ambaye alionekana kupiga stori kwa muda mrefu na kocha huyo mpya.

Mazungumzo yalipomalizika, walipeana mikono watu wote wa benchi la ufundi na waliingia uwanjani pamoja na wachezaji mazoezi yakaanza.

Mazoezi ya mwanzo yalionekana kuwa ya kurudisha utimamu wa mwili uliopotea baada ya mapumziko, huku kwa vipindi fulani wachezaji wakichezea mipira.

Kocha huyo alisema anatamani kufanya kazi saa 24 ili kuhakikisha anaiimarisha timu hiyo kwani ina wachezaji bora.

"Nina imani bado nina vitu vingi vya kuwaongezea kimbinu na kiufundi, nadhani changamoto kubwa itakuwa ni kujifunza hukusu ligi hii, nimepewa taarifa kuwa kuna baadhi ya viwanja si vizuri eneo la kuchezea, inabidi ubadili mbinu ili uweze kupata matokeo mazuri, hivyo naendelea kutazama mechi ilizocheza Yanga huko nyuma kwenye viwanja hivyo ili nijifunze mengi na vitu vipya," alisema kocha huyo.

Kocha huyo alitangazwa mwishoni mwa wiki kuchukua nafasi ya Miguel Gamondi raia wa Argentina ambaye aliondolewa kwenye kikosi hicho kwa sababu ambazo hazijawekwa wazi na uongozi, lakini wengi wakihusisha na vipigo viwili mfululizo ilivyovipata dhidi ya Azam FC kwa bao 1-0 na Tabora United mabao 3-1.

Klabu hiyo pia ilimtanga Kodro kutwaa nafasi ya aliyekuwa Kocha Msaidizi, Moussa N'Daw, raia wa Senegal, aliyetimuliwa pamoja na bosi wake.

Aidha, Yanga imemtangaza, Abdulhamid Moallin, aliyekuwa Kocha Mkuu wa KMC, kuwa Mkurugenzi wa Ufundi wa klabu hiyo.