KLABU za Simba, Yanga na TP Mazembe zimetajwa kupeleka ofa katika klabu ya Fountain Gate kwa ajili ya kuhitaji nyota wa timu hiyo katika dirisha dogo la usajili lililofunguliwa hivi karibuni, imefahamika.
Habari kutoka Fointain Gate zinasema Simba imepiga hodi ikitaka huduma ya straika, Edgar William wakati Yanga wanamhitaji beki wa kushoto, Laurian Makame na TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, imeweka nia ya kumsajili, Selemani Mwalimu.
Chanzo hicho kimesema klabu hizo zimewasilisha ofa zao na tayari zimeanza kufanyiwa kazi.
"Hapa kuna ofa tatu, sasa kama tutazikubali zote ili na sisi tufanye usajili kipindi hiki, au tutoe mchezaji mmoja wengine tuwaache au wawili. Na pia tunataka kuangalia ni sehemu gani ambazo tukitoa wachezaji hatutoathirika zaidi, ni vitu vingine tu tutaangalia kabla ya kufanya uamuzi," kilisema chanzo chetu.
Kiliongeza TP Mazembe inamhitaji Mwalimu ambaye tayari ameshafunga mabao matano mpaka sasa katika Ligi Kuu Tanzania Bara, akishika nafasi ya pili nyuma ya Elvis Rupia wa Singida Black Stars mwenye mabao saba.
"Mazembe wamebaini wanahitaji kujiimarisha, wameona wanaudhaifu kwenye eneo la ushambuliaji ambalo linawagharimu kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, hatua ya makundi," kiliongeza chanzo hicho.
Edgar, ambaye pia ana mabao matano anahitajiwa na Simba ili kwenda kutoa ushindani kwa mastraika wengine akiwamo, Steven Mukwala na Leonel Ateba, huku Makame akitakiwa na Yanga ili kwenda kuimarisha eneo la beki wa pembeni.
Akizungumzia hilo, Kocha Mkuu wa Fountain Gate, Mohamed Muya, alisema binafsi hajapata taarifa yoyote kutoka kwa viongozi kama wamepokea ofa ya kutakiwa wachezaji hao.
Muya alisema hana hofu yoyote kama wachezaji hao wataondoka, na badala yake watatengeneza nyota wapya na hiyo ndiyo 'biashara' ya soka inavyokwenda.
"Kazi yetu walimu ni kutengeneza wachezaji, ukiangalia tulisalia na wachezaji sita tu wakati tunaitwa Singida Big Stars, baada ya wengi kupelekewa Ihefu FC ambayo ilibadilishwa ikawa Singida Black Stars, lakini tulipata wengine tukawatengeneza na watu wameanza kuwatolea macho.
Hata sisi tunawaombea vijana tunaowatengeneza wasonge mbele, waende mbali wapate mafanikio, sijapata taarifa rasmi kutoka kwa viongozi, lakini kama ni hivyo tunawaombea baraka, Mungu awajalie wanakokwenda, tutapata wengine nao watakuwa kama hawa," alisema kocha huyo.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED