BAADA ya kufanya sherehe ya wiki nzima kwa kuifunga Yanga mabao 3-1 Novemba 7, mwaka huu, sasa kikosi cha Tabora United kimeanza rasmi mazoezi kujiandaa na mchezo ujao dhidi ya Singida Black Stars huku kikitamba kuwa timu hiyo itakipata kile ambacho kiliwakuta wenzao katika mechi hiyo itakayopigwa Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi Jumapili ijayo.
Ofisa Habari wa klabu hiyo, Christina Mwagala, amesema wachezaji wote wa timu hiyo walianza mazoezi juzi, isipokuwa Salum Chuku ambaye ni majeruhi na wamekuwa na ari na nguvu kubwa baada ya kuonekana kuwa mashujaa kwa kuifunga Yanga.
"Baada ya kupata heshima kubwa na zawadi kutoka kwa watu mbalimbali na mashabiki wa soka nchini, wachezaji wa Tabora United wameanza mazoezi kwa ari na nguvu kubwa, tunachohitaji kwa sasa ni kuendeleza mlolongo wa ushindi, hatukuanza vizuri ligi, lakini tumeshinda mechi tatu mfululizo, tunataka tuendeleze ushindi na lengo letu mwisho wa msimu tuwe ndani ya zile timu nne za juu, ndiyo tunalohitaji msimu huu," alisema Mwagala.
Aliitahadharisha Singida Black Stars kuwa kama wakija vibaya, basi kile ambacho kiliwakuta Yanga nao kitawakuta na huenda idadi ya mabao ikawa kubwa zaidi.
"Hapa tunaandaa dozi kwa Singida Black Stars, tunawaambia wakija ovyo, watakutana na alichokutana nacho Yanga, na yeye vile vile kitakwenda kumkuta, kwa sababu mchezo huu unachezwa nyumbani na mashabiki wetu wengi watahudhuria kwani wamehamasika sana baada ya ushindi dhidi ya Yanga, kutokana na hilo hatutaki kuwapa tena huzuni na kuwapoteza mashabiki wetu," alisema Ofisa Habari huyo.
Baada ya kutofanya vizuri kwenye michezo kadhaa ya Ligi Kuu kiasi cha kumfukuza kocha wake, Francis Kimanzi, hasa baada ya kuchapwa mabao 4-2 dhidi ya JKT Tanzania, Oktoba 18, mwaka huu, timu hiyo ilishinda mechi tatu mfululizo, ikiifunga Pamba Jiji bao 1-0, Mashujaa FC 1-0, kabla ya kuitwanga Yanga mabao 3-1.
Ipo nafasi ya sita kwenye msimamo wa Ligi Kuu, ikiwa na pointi 17, ikicheza mechi 11, ikishinda tano, sare mbili na kupoteza nne.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED