JUMLA ya timu tisa za Ligi Kuu na 10 za Ligi ya Championship zimetinga hatua ya raundi ya nne ya Kombe la Shirikisho la Mpira wa Miguu Nchini (TFF), maarufu Kombe la FA zilizochezwa wiki iliyomalizika kwa siku tano mfululizo.
Jumla ya michezo 19 imechezwa, kasoro timu za Simba na Yanga ambazo zipo kwenye hekaheka ya michezo ya kimataifa.
Mechi hizo ni za kusaka ubingwa kwa ajili ya kucheza michuano ya Kombe la Shirikisho barani Afrika msimu ujao.
Tukianza na timu 10 za Championship zilizotinga raundi nne ni Transit Camp, iliyoifunga Gunners mabao 3-2, mechi ikichezwa Uwanja wa Mabatini, Mlandizi mkoani Pwani, Biashara United ikiitandika TRA mabao 5-0, mchezo uliopigwa Uwanja wa Karume, Musoma mkoani Mara.
Songea United nayo ilipata ushindi kwa mikwaju ya penalti 3-2 dhidi ya Kidulu FC, baada ya sare ya mabao 2-2 katika Uwanja wa Majimaji, Songea, Cosmopolitan ikishinda 2-0 dhidi ya Nyota FC Uwanja wa Mabatini, Polisi Tanzania ikaidundua Bukombe FC, bao 1-0, Uwanja wa Ushirika, Moshi.
Stand United pia iliichapa Don Bosco mabao 2-0, Uwanja wa Kambarage, Mbeya City ikaifunga Mapinduzi, mabao 2-1, Uwanja wa Sokoine, Mbeya, Green Warriors ikaichapa Hausung kwa penalti 4-2, baada ya sare ya bao 1-1, Mabatini, na TMA, ikaiangamiza Leopards FC mabao 5-1, Sheikh Amri Abeid jijini Arusha.
Kwa upande wa timu za Ligi Kuu, Singida Black Stars ilishinda 2-0 dhidi ya Magnet katika Uwanja wa Liti mkoani Singida, Mashujaa ikaitwanga Tukuyu Stars, mabao 3-0 Uwanja wa Lake Tanganyika, Kigoma, Pamba ikashinda bao 1-0, dhidi ya Moro Kids, CCm Kirumba jijini Mwanza, Coastal Union ikashinda 4-0 dhidi ya Stand FC Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha.
Azam nayo ikaifunga Iringa Sports mabao 4-0 Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Namungo ikashinda 2-1 dhidi ya Tanesco FC, Majaliwa, Ruwanga mkoani Lindi, JKT Tanzania ikipata ushindi wa mabao 5-1 dhidi ya Igunga, Uwanja wa Jenerali Isamuhyo, Dar es Salaam.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED