Yanga kufa na TP Mazembe leo

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 08:56 AM Dec 14 2024
Yanga kufa na TP Mazembe leo.
Picha:Yanga
Yanga kufa na TP Mazembe leo.

KOCHA Mkuu wa Yanga, Sead Ramovic, amesema watafanya kila njia kuhakikisha wanapata ushindi wa ugenini leo dhidi ya TP Mazembe ili kujiweka kwenye mazingira mazuri ya kuwa na matumaini ya kuingia hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kutoka Kundi A.

Yanga leo itashuka ugenini, Uwanja wa Mazembe, Lubumbashi, saa 10:00 jioni kucheza mchezo wa raundi ya tatu ambapo inahitaji ushindi kwa udi na uvumba ili kurejesha matumaini ya kuelekea kwenye robo fainali ya michuano hiyo.

Ramovic, amesema ameshaandaa mfumo wa kucheza mchezo wa leo na anaamini wachezaji wake watautekeleza kwa vitendo wakiwa ndani ya uwanja.

"Tunacheza na timu ngumu, inayocheza soka la moja kwa moja. Tutajitahidi kumiliki mechi, lakini kuna wakati tutapoteza mipira nimeshatengeneza mfumo unaotuelekeza nini tutafanya ili kuinyang'anya haraka na hii ni kazi ya timu nzima kurudi nyuma na kusaka mpira miguuni mwa wapinzani na kushambulia kwa kasi, naamini tunakwenda kufanya vizuri," alisema kocha huyo.

Yanga inacheza mechi ya leo ikiwa haina pointi yoyote, ikiwa imecheza mechi mbili na kupoteza zote kwa mabao 2-0, dhidi ya Al Hilal Omdurman ya Sudan na MC Alger ya Algeria.

Kiungo mshambuliaji wa timu hiyo ambaye wakati mwingine hucheza kama winga, Maxi Nzengeli, amesema pamoja na kwamba wamepitia kwenye mazingira magumu ya kupoteza mechi kwa siku za karibuni lakini bado wachezaji wameendelea kupambana kwenye mazoezi na wanaamini watafanya vizuri kwani timu ina wachezaji wengi waliocheza na TP Mazembe mwaka jana katika mechi ya Kombe la Shirikisho Afrika hatua ya makundi.

"Tumepitia katika mazingira magumu kutokana na matokeo mabaya, lakini sisi kama wachezaji tumeendelea kupambana na mazoezi, tuliokuja kucheza ni kwa asilimia kubwa ni wale wale tuliocheza dhidi ya TP Mazembe kwenye Kombe la Shirikisho mwaka jana, tukashinda michezo yote miwili dhidi yao," alisema Ramovic.

Yanga iliifunga TP Mazembe mabao 3-1 katika mchezo wa kwanza uliochezwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, Februari 19 mwaka jana, kabla ya kushinda tena kwenye uwanja watakaochezea leo bao 1-0, mchezo ukipigwa Aprili 2 mwaka jana.

TP Mazembe yenyewe ina pointi moja tu iliyoipata ilipocheza dhidi ya MC Alger kwa kutoka suluhu, hivyo nayo inahitaji pointi tatu ili kuweka hai matumaini ya kusonga mbele kwenye hatua inayofuata kwenye kundi hilo ambapo mechi nyingine ya kundi hilo kati ya MC Alger itakayokuwa nyumbani dhidi ya Al Hilal, itachezwa leo saa 4:00 usiku kwa saa za Tanzania.