Mama,babalishe usafi ni njia kuvuna wateja

By Sabato Kasika , Nipashe
Published at 10:22 AM Aug 16 2024
Mama Lishe.
Picha: Mtandao
Mama Lishe.

AJIRA binafsi ndiyo habari ya mjini tena zimeshika nafasi kubwa. Watu wakijituma kufanya shughuli mbalimbali, ikiwamo biashara ya kuuza chakula au ya mama na babalishe iliyosambaa maeneo ya mijini hadi vijijini.

Hata hivyo, kundi la wauza chakula , limekuwa likikabiliwa na changamoto ya uchafu  katika biashara, jambo linalohatarisha afya za wateja wao.
 
 Baadhi yao huandaa vyakula katika mazingira ambayo si salama kwa wateja, wanasahau kwamba, kupika chakula na kukiweka katika mazingira safi, ni kuvuta wateja wakiwamo wenye pochi nene.
 
 Hivyo, ni vyema kutambua kuwa, wakati mwingine, mamalishe wanaweza kufukuza wateja wao wenyewe kutokana na mazingira ya kuandalia vyakula kuwa machafu .
 
 Baadhi yao huandaa vyakula katika eneo ambalo mbele kuna rundo la taka wanazozalisha, wapo inzi na wengine humwaga maji waliyooshea vyombo vya vyakula, katika mitaro iliyo karibu na eneo la biashara na kuongeza harufu mbaya kila siku.
 
 Kuzingatia usafi katika maeneo ya biashara na kufuata kanuni za afya ikiwamo kuweka vitunzia taka, sehemu ya kuhifadhia maji na kuacha kumwaga maji machafu ovyo ni jambo la msingi.
 
 Usafi binafsi kwa wafanyabishara wanaojihusisha na biashara ya kuuza vyakula ni moja ya mambo ya msingi ya kuzingatia ili kufanya biashara hiyo katika hali ya mvuto na afya bora.
 
 Ikumbukwe kuwa, usafi si wa nyumbani au mwili pekee, bali hata kwenye mazingira yanayozunguka eneo la biashara, hivyo, kuanzisha biashara kama ya chakula, huku eneo la kufanyia biashara likiwa na maji machafu au uchafu wa aina yoyote, ni hatari kwake na kwa wateja.
 
 Katika mazingira hayo, ni rahisi kukimbiwa na wateja. Ikumbukwe kuwa uchafu hukaribisha nzi, ambao husambaza magonjwa, kama vile kipindupindu na magojwa mengine ya tumbo.
 
 Uchafu hauna faida yoyote, hivyo, wafanyabiashara hawana budi kuhakikisha wanatunza na kusafisha mazingira ya biashara zao kila siku, na kuendelea kuvutia wateja, ili wajipatie kipato cha kutosha.
 
 Kwa kawaida ni kwamba, hakuna mteja anayejitambua ambaye anaweza  kwenda kununua bidhaa fulani, katika mazingira machafu hata kama bidhaa hiyo iko karibu, badala yake atakwenda kuitafuta mbali. Hivyo, mamalishe, babalishe kumbukeni usafi ni kivutio kwa wateja.
 
 Hivyo, sio vibaya maofisa biashara na wanaohusika na afya wakawatembelea mara kwa mara wafanyabishara na kuwaelimisha umuhimu wa kufanya biashara bila kuhatarisha afya za wateja.
 
 Lakini pia, wafanyabiashara hao wanatakiwa kuwa na mavazi vimori au aproni  na kofia, kuzingatia usafi binafsi katika wa mazingira yanayowazunguka.
 
 Vilevile, mamalishe na babalishe, wasichukulie suala la usafi katika biashara zao kama jambo la hiari, bali kila mmoja ausimamie katika eneo lake, vinginevyo wanaweza kukimbiwa na wateja bila kujua chanzo.
 
 Kila mfanyabiashara anayejua umuhimu wa usafi, ni vyema asaidie kuwafundisha wenzake, ili wote wauzingatie katika maeneo yao ya biashara ili wasikimbiwe na wateja na kudhani wanalogwa kumbe ni wachafu.
 
 Inawezekana wapo baadhi yao wanaoamini kuwa kukimbiwa na wateja katika biashara zao ni kutokana na mkosi au kurogwa na kwenda kutafuta dawa kwa waganga, lakini kumbe chanzo ni wao wenyewe.
 
 Watu wa aina ni vyema wakatambua kuwa ubunifu ni wa muhimu ili kuvutia wateja, lakini pia kuzingatia usafi ni jambo lingine lenye uzito wake  katika biashara ya mamalishe na babalishe.
 
 Ninaamini  kila mmoja akiwa na kifaa cha kutunzia taka na kukitumia itakiwavyo, itakuwa rahisi kudhibiti utupaji taka ovyo kwenye eneo la biashara kama ilivyo sasa.
 
 Lakini kikubwa zaidi ambacho kingefanyika, ni kuwatengezea maeneo ya biashara na kuwawekea miundombinu  muhimu  pamoja na  uongozi utakaosimamia kila kitu likiwamo suala la usafi.