Waamuzi msitake kuitoa 'dabi' ya utani kwenda kuwa ya uadui

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 11:57 AM Oct 21 2024
Mwamuzi Ramadhan Kayoko
Picha:Mtandao
Mwamuzi Ramadhan Kayoko

TOKA juzi huwezi kuwaambia baadhi ya mashabiki wa Simba kuwa dabi dhidi ya Yanga ni utani wa jadi akakuelewa.

Ni kwa sababu wanaona hawakufungwa kihalali. Walipaswa kama si kushinda basi angalau watoke sare kutokana na kunyimwa penalti mbili ambazo wao wanadai ni halali. Marudio ya picha za televisheni yanaonesha hivyo.

Ramadhani Kayoko hakuona, hakuwa makini au alipotezea na kusababisha mashabiki wa Simba kucharuka hasa baada ya kufungwa bao dakika za jioni.

Kumbukumbu zinanipeleka katika mchezo uliopita ambako pia mashabiki wa Simba walilalamika kunyimwa penalti ambayo ingeweza kuwapa sare kwenye mchezo wao dhidi ya Yanga na kuwapeleka kwenye mikwaju ya penalti katika mchezo wa nusu fainali ya Ngao ya Jamii.

Kwa sasa mashabiki wa Simba wanachoamini ni kwamba kumekuwa na uonevu kwa timu yao kwani matukio mengi ya makosa ya waamuzi yamekuwa yakiangukia kwao.

Mioyoni wameanza kuitoa mechi yao na Yanga kama utani wa jadi na kutaka kuiweka kwenye uadui kwani wanaona pamoja na jitihada wanazozifanya, lakini wanaangushwa na maamuzi ya waamuzi.

Ikumbukwe mechi za Simba na Yanga zilianza rasmi kuchezwa 1937, baada ya timu zote mbili kuwa tayari zimeanzishwa.

Yanga ilianzishwa rasmi Februari 11, 1935 na Simba ilianzishwa 1936, na zilikuwa zikicheza michezo kwenye vikombe mbalimbali jijini Dar es Salaam, kabla ya kuanzishwa rasmi kwa Ligi Kuu, iliyotambulika wakati huo kama Ligi ya Taifa mwaka 1965, wakati huo bado ikiitwa Sunderland.

Kwa miaka hiyo yote mechi za dabi zimekuwa za kitamaduni zaidi na ni tofauti na dabi zingine katika nchi zingine ambazo zimekuwa na uhasama kiasi cha watu kuuana.

Hapa nchini ni mechi za utani wa jadi na unaweza kuona mashabiki wa Yanga wakishinda wanaweza kuwanunulia chakula na vinywaji wenzao wa Simba huku wakiwazodoa, kitu ambacho unaweza usikikute nchi zingine.

Utani huu ndiyo umeweza kuifanya dabi hii kuwa bora na maarufu zaidi na kuua zile za Gor Mahia na AFC Leopards ya Kenya na hata SC Villa na Experess za Uganda.

Dabi ya Tanzania ndiyo ya ajabu zaidi kwani familia moja inaweza kugawanyika wengine wakawa Simba na wengine Yanga, tofauti na baadhi ya nchi ambazo familia yote na hata majirani wanakuwa ni timu moja kwa sababu wanashangilia timu inayotoka ukanda huo tu.

Yaani kama timu inaitwa Kinondoni FC, basi watu wote wa huko wanakuwa mashabiki wa timu hiyo, hivyo familia nzima na wanaowazunguka wote mnakuwa timu moja.

Pamoja na yote hayo, watu wameendelea kuwa wamoja kutokana na uadilifu mkubwa wa waamuzi katika michezo ambayo wanakutana.

Hata Yanga walipofungwa mabao 6-0 mwaka 1977 hakukuwa na tuhuma za mwamuzi, 5-0 mwaka 2012, hata Simba walipofungwa mabao 5-1 msimu uliopita, hakuna shabiki yoyote aliyelia na refa zaidi ya kudai wachezaji wao wameshachoka na hilo liliwafanya kuondoa wengi.

Kwa maana hiyo kilio cha wanachama na mashabiki wa Simba kisipuuzwe, kwani uchezeshaji huu unaweza kuwafanya waone Yanga ni maadui zao na si watani wa jadi tena.

Hili litafutika kwa Shirikisho la Mpira wa Miguu (TFF), na Bodi ya Ligi kukaa chini na kusaka mustakabali wa hili, dabi ichezeshwe kwa haki na ionekane kuwa imetendeka, ili aliyefungwa ampe mwenzake mkono, vinginevyo kunaweza kuzuka matatizo mbele ya safari.

Imetosha kuona mechi za dabi za siku za karibuni waamuzi ndiyo 'wanaotrendi' zaidi na kuzungumzwa na mashabiki na wachambuzi kuliko uwezo wa wachezaji wanaouonesha uwanjani.

Kwa haya wanayofanya waamuzi wanafanya hata mashabiki kupendekeza sasa hata mwamuzi awe na nafasi ya kuchaguliwa katika Tuzo ya Mchezaji Bora wa Mechi ('Man of The Match'), kutokana tu na tabia yao ya kuzifinyanga sheria 17 za soka kwa kuamua matokeo.

TFF na Bodi ya Ligi, wanapaswa kuilinda tunu ya dabi ya Kariakoo iendelee kuwa ya utani wa jadi badala ya uadui kwa kuhakikisha mpira unachezeshwa kwa haki bila kumpendelea yoyote yule.

Mashabiki wengi wa soka duniani huwa wanaridhika wanapofungwa kihalali, lakini si kwa utata kama mechi hii.