USAFI ni jambo jema kwa vile kwenye taka kuna wadudu kuanzia wanaotambaa hadi wanaoruka lakini pia kuna harufu.
Lakini inashangaza mfanyabiashara yuko pembeni anauza bila kujali kuwa anapouzia ni pachafu na ni kero kwake na wale anaowahudumia.
Katika maeneo yenye mikusanyiko ya watu, ndiko kuliko na fursa. Utakubaliana nami unaposhuhudia idadi kubwa ya watu hususan maeneo yenye shughuli muhimu.
Ni kwenye masoko, vituo vya daladala na mabasi ya masafa, viwanja vya michezo na karibu na shule.
Maeneo haya wajasiriamali wengi huyatumia kama vyanzo vya mauzo kwa kuwa katika idadi hii kila mmoja atakuwa na mahitaji yake.
Wafanyabiashara hawa ambao wengi wao wapo katika kundi la wajasiriamali wadogo, utakutana na wauza vyakula, vinywaji, bidhaa za majumbani, vifaa vya kielektroniki, nguo, viatu na mahitaji ya shuleni.
Pamoja na serikali kutoa vibali na baadhi ya wajasiriamali hawa kupatiwa vitambulisho kufanya biashara maeneo haya, kuna changamoto ya usafi na utunzaji wa mazingira yanayozunguka maeneo haya.
Ukifika vituo vya daladala, mfano Kariakoo, Makumbusho, Gongo la Mboto vyote vya Dar es Salaam utashuhudia tatizo hilo kwani wengi kwenye biashara zao hawajali usafi cha muhimu pesa kwanza.
Pia maeneo ya soko Tandika, Kariakoo, Manzese, Urafiki, Tandale na Buguruni Dar es Salaam, unakutana na uchafu usiopendeza machoni.
Jamani kumbukeni mtu ni afya, kuzitunza afya za wateja na unayeuza bidhaa ni kitu muhimu. Wachuuza wanapoanza biashara asubuhi, hawafanyi usafi utadhani ufagio ni adui.
Wamekaa pembeni ya rundo la taka za matikititi, machungwa, maganda ya mahindi, ndizi, vifungashio, maboksi na majini mabichi yanayofungia bidhaa.
Ingekuwa ni bora fursa iendane na wajibu, sababu fursa wamepewa wajasiriamali hawa ambao kundi kubwa ni vijana, siku hizi mjini wanasema 'kujiongeza'.
Wafanyabiashara mjiongeze katika maeneo yenu ya biashara kwa kila mmoja kuwa na chombo cha kuhifadhi taka yaani vikapu, ndoo au beseni kutunza taka zenu, si sawa hata kidogo uzalishe uchafu tena kila dakika usubiri waje wakufagilie.
Kuna ambao watasema tunalipa ushuru. Ni sawa ushuru unalipwa, lakini akija mfanya usafi akute pa kuanzia, labda taka zimetunzwa mahali fulani atazikusanya na kumalizia kufagia.
Ni sawa na kusema ukilipia ushuru, uache eneo chafu au mazingira machafu. Mbona katika vyoo vya kulipia utalipia gharama ya Sh. 300 hadi 500 lakini baada ya kutumia choo iwe haja ndogo au kubwa, utaacha umemwagia maji au kusafi.
Ni wachache wasio na uelewa wakaacha choo kichafu na kumfanya anayeingia baada yako arudi nyuma kama ameona chatu chooni.
Jamani hata wanaokuja kufanya usafi katika maeneo yenu ya biashara iwe soko au vituo vya daladala ni watu kama wengine, ambao wanahitaji kukuta utaratibu uliowekwa na wewe mzalisha uchafu kisha zikabebwa na gari taka hadi Pugu dampo.
Kituo kipya cha Mwenge, Dar es Salaam, ni kizuri na usafi pia upo, kitakaposhamiri kwa kutoa huduma je, usafi utaimarika?.
Wajasiriamali, wafanyabiashara kuweni rafiki wa mazingira kwa kuwa wasafi na muwe na vyombo vya kuhifadhia taka ngumu, na si kutupa taka barabarani.
Hii inawachanganya hata wafagizi wa barabara ambao yeye huja na toroli, mfagio na koleo ili aweze kuzoa mchanga akishafagia, huchanganyikiwa anakutana na maganda ya miwa, ndizi au makopo akijiuliza azoe mchanga au taka ngumu.
Wafanyabiashara hiyo ndio ajira ambayo isiyo rasmi lakini inatambulika kwa kuziwezesha familia zenu kupata mahitaji na ni maendeleo pia kwa nchi, lakini kumbukeni mtu ni afya na maofisa afya wachukue hatua.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED