MAOFISA uandikishaji na waratibu wa uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura 520, walioteuliwa na Tume Huru ya Uchaguzi nchini (INEC), kutoka kwenye Magereza yote wamekula kiapo leo Juni 22, 2025 kuanza utekelezaji wa jukumu hilo.
Kwa mara ya kwanza nchini Magereza yote wafungwa wake wenye kifungo cha chini ya miezi sita na Mahabusu wenye sifa watashiriki mchakato wa kikatiba wa kupiga kura na kuchagua viongozi wao kwenye uchaguizi mkuu 2025.
Baada ya maofisa hao kula kiapo, uandikishaji na uboreshaji wa daftari la wapiga kura unatarajia kuanza katika Magereza yote nchini Juni 28 hadi Julai 4, 2025 kwa kuwaandikisha wafungwa na mahabusu wenye sifa za kushiriki uchaguzi mkuu kwa mujibu wa sheria.
Mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi nchini (INEC), Jaji wa Mahakama ya Rufani Jaji Jacobs Mwambegele, akizungumza jijini Dodoma na maofisa hao mara baada ya kula kiapo amewapongeza kwa kuteuliwa kushiriki jukumu hilo la kikatiba.
Aidha, Kiapo hicho hicho kimetolewa pamoja na mafunzo kwa waandishi wa wasaidizi na waendesha vifaa vya biometriki ambao watatekeleza jukumu hilo la kikatiba.
“Katika semina hii ni matumaini yangu kuwa kila mmoja wenu atapata elimu na ujuzi wa kutosha kuteleza majukumu yake kwa ufanisi mkubwa wakati wa uandikishaji wapiga kura kwenye Magereza yetu nchini.
“Mafunzo haya yatafanyika kwa nadharia na vitendo ambayo yatahusisha ujazaji fomu mbalimbali matumizi ya mfumo wa uandikishaji wapiga kura pamoja na kupata uelewa wa kina wa vifaa vitakanyotumika wakati wa zoezi hili,”amesema Jaji Mwambegele
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED