WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Hamad Masauni amewahimiza Watanzania kutumia nishati safi kupikia, ikiwa ni mkakati wa kupambana na mabadiliko ya tabianchi, uharibifu wa mazingira na kuhifadhi viumbe hai.
Aliyasema hayo mwishoni mwa wiki, jijini Dar es Salaam, wakati wa futari aliyoiandaa pamoja na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), kwa wadau mbalimbali.
“Tunapohimiza kuhusu mazingira hatufanyi haya yote kwa ajili yetu wenyewe, bali kwa vizazi vitakavyokuja baada yetu kwa maana ya watoto na wajukuu zetu.
Alisema wadau mbalimbali wana wajibu wa kutengeneza dunia endelevu na yenye maelewano kwa wote, huku akisisitiza umuhimu wa kulinda rasilimali zilizopo kwa kuhakikisha zinaendelea kuwapo, kwa ajili ya watoto na vizazi vijavyo.
Pia, alisema kila mtu anatakiwa kuzingatia jinsi matendo yake, hata yawe madogo kiasi gani katika uhifadhi wa mazingira, kwa kuwa yanaweza kuwa na athari kubwa sana kwa mazingira.
Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Dk. Immaculate Semesi alisema kazi inayofanywa na wadau mbalimbali katika kuhifadhi, kulinda na kusimamia mazingira, ni faida kubwa kwa mazingira katika kutimiza maandiko ya vitabu vitakatifu.
“Sote tunajua Tanzania imebarikiwa kuwa na maliasili na mifumo ikolojia ya kipekee ambayo ni pamoja na aina nyingi za mimea, wanyama, wadudu, ndege tunatakiwa kuhakikisha tunapunguza athari za mabadiliko ya tabianchi.
“Kudhibiti shughuli za kibinadamu zinazoharibu mazingira kama uchimbaji madini, ufugaji na kilimo visivyo endelevu na ukataji mkubwa wa misitu,” alisema.
Alisema juhudi za pamoja ni kuhakikisha kwamba, aina hizo tofauti za uharibifu zinapunguzwa ama kumalizwa kabisa na kwamba hilo ndilo lengo ambalo serikali kupitia NEMC inajitahidi kufikia.
Alisema tukio hilo lililopangwa kufanyika katika Viwanja vya Mnazi Mmoja, jijini Dar es Salaam ni mahususi kwa kuyaleta pamoja makundi mbalimbali ya wadau wa mazingira, kwa lengo la kuangazia umuhimu wa usimamizi endelevu wa taka na kukuza uchumi mzunguko (promote a circular economy).
Alisema kauli mbiu ya mwaka huu ni "Kufikia lengo la taka sifuri katika masuala ya mitindo na nguo" na kauli mbiu ya Kitaifa ni "TAKA NI FURSA".
Aliongeza kwamba mbali na jitihada zinazofanywa, serikali imepiga hatua katika kuhakikisha mazingira yanalindwa na yanahifadhiwa vizuri, ili kuendelea kutoa huduma na bidhaa zinazohitajika kwa kufanya tathmini ya athari za kimazingira na kijamii.
Pia, alisema wanafanya tafiti za mazingira na usimamizi wa maeneo maalum, kusaidia uhamasishaji na programu za kuelimisha umma na kutambua kuwa mazingira ni suala mtambuka, majukumu ya usimamizi wa mazingira yanatakiwa kutekelezwa na takriban kila sekta kupitia sheria, kanuni, mikakati na mipango ya kisekta.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED