Papa Francis aruhusiwa kutoka hospitali Gemeli

By Maulid Mmbaga , Nipashe Jumapili
Published at 05:20 PM Mar 23 2025
Papa Francis
Picha: Mtandao
Papa Francis

KIONGOZI wa Kanisa Katoliki Duniani, Papa Francis, ameruhusiwa kwenda nyumbani baada ya kuuguzwa hospitalini kwa zaidi ya mwezi mmoja.

Alilazwa kutokana na changamoto ya mfumo wa kupumua pamoja na nimonia au kichomi.

Papa Francis, alilazwa hospital February 14, mwaka huu. Kwa mujibu wa madaktari waliokuwa wakimtibu katika hospitali ya Gemeli, mjini Roma, Papa ataondoka hospitalini leo.

Atarejea katika makazi yake rasmi huko Vatican ambako anatarajiwa kupata mapumziko ya ndani kwa muda wa miezi miwili.

Pia imeelezwa kuwa atawabariki waumini waliokusanyika nje ya hospitali hiyo kumuombea apate afueni, kisha ataondoka kuelekea kwenye makazi yake ambako ataangaliwa kwa ukaribu na madaktari wake.

Imeelezwa kuwa kiongozi huyo hatoweza kujichanganya na watu wengi, kwa muda wa miezi miwili hadi pale afya yake itakapohakikishwa kuwa salama kabisa.

Papa Francis mwenye umri wa miaka 88 amekuwa hospitalini kwa wiki tano hivi, na katika muda huo alikabiliwa na changamoto zaidi za kiafya mara mbili ambapo madaktari wanasema maisha yake yalikuwa hatarini.

Daktari Sergio Alfieri, ambaye ni mmoja wa madaktari wanaomtibu Papa Francis amesema kwamba wamefurahia hali ya kwamba Papa atarejea nyumbani.

Aidha, amefafanua kwamba, “wagonjwa wanaouguwa hali mbaya ya nimonia hupoteza sauti hasa wakiwa wenye umri mkubwa, kwa hivyo itachukuwa muda kwa sauti ya mgonjwa kurejea hali ya kawaida.”

Siku ya Ijumaa, Kadinali Victor Fernandez aliambia wanahabari kwamba Papa alipoteza hewa ya Oksijeni mara kwa mara na idadi kubwa ya hewa hiyo hukausha viungo mwilini hasa kwenye koo, na kwa sababu ya hilo Papa atalazimika kujifunza kuzungumza upya.

Wiki chache zilizopita Wakristo waliadhimisha Jumatano ya Majivu kwa ibada maalum, ambako Papa hakuhudhuria kutokana na hali yake ya kiafya.

BBC